Na Lilian Lundo – MAELEZO
ZAIDI ya wafanyabiashara 100 kutoka Tanzania na Kongo wanatarajia kushiriki kongamano la biashara litakalofanyika Lubumbashi Kongo Septemba 22 mwaka huu.
Lengo la Kongamano hilo ni kuimarisha uhusiano wa kibiashara, kuongeza kiasi cha mauzo ya nje na kuboreshwa mazingira mazuri ya biashara kati ya nchi hizo mbili.
“Wafanyabiashara wa Tanzania wana nafasi kubwa ya kupata soko nchini Kongo, kutokana na nchi hiyo kutegemea bidhaa nyingi kutoka Tanzania kama vile samaki wabichi na wakavu kutokana na nchi hiyo kutokuwa na bahari,” alifafanua Afisa biashara wa TANTRADE Bi. Getrude Ngwesheni.
Aliendelea kwa kusema kuwa Kongo wanaongea lugha ya kiswahili kuwasiliana, lugha ambayo inatumika na watanzania wengi, hivyo itarahisisha mawasiliano katika shughuli za biashara.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kongamano hilo kutoka Chama cha wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Bi. Anna Msonsa amesema kuwa kongamano hilo linatoa fursa kwa wafanyabiashara wote kuanzia wa chini mpaka wale wakubwa na kuwataka wafanyabiashara kujitokeza kwa wingi kushiriki kongamano hilo.
Akitoa maelezo ya namna ya kushiriki Kongamano hilo Afisa Miradi kutoka Kampuni ya 361 Bi. Naomi Godwin amesema kuwa wafanyabiashara wanatakiwa kujaza fomu ambazo zinapatika katika ofisi za 361 digrii zilizoko Msasani pamoja na ofisi za TCCIA na TANTRADE au kwa kutembelea tovuti ya www.tanzaniadrc.com.
Aidha, kongamano hilo limeandaliwa na Ubalozi wa Tanzania Kongo, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Chama cha wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Shirikisho la wafanyabiashara wa Kongo (FEC), Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA), Taasisi ya Sekta Binafsi Nchi Tanzania (TPSF), Kampuni ya 361 Degrees na mdhamini mkuu ambaye ni Taasisi ya GSM Foundation.