Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA), Stephen Ngatunga (kushoto), akizungumza katika mkutano huo. Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa TAT, Omar Kiponza.
Makamu Mwenyekiti wa TAT, Omar Kiponza (kulia), akizungumza katika mkutano huo.
Rais wa Chama cha Wasafirishaji Tanzania (TAT), Zacharia Hans Pope (wa pili kushoto), akiwa na viongozi wengine meza kuu.
Na Dotto Mwaibale
WADAU wa usafirishaji wa mizigo kwenda nje ya nchi wameiomba serikali kusimamisha kwa muda sheria ya tozo la VAT katika mizigo inayosafirishwa ili kulinusuru taifa kiuchumi.
Ombi hilo limetolewa na Rais wa Chama cha Wasafirishaji Tanzania (TAT), Zacharia Hans Pope wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi kuzungumzia changamoto ya sheria hiyo.
“Sheria hii haina manufaa yoyote katika kuinua uchumi wa nchi yetu kwani imesabisha mizigo kupungua katika bandari yetu kutokana na wadau wa usafirishaji kuanza kutumia bandari za nchi jirani kwa kuogopa kulipa kodi hiyo ya mizigo” alisema Hans Pope.
Alisema hivi sasa katika bandari ya Dar es Salaam kumekuwa na upungufu mkubwa wa mizigo jambo lililosababisha magari ya mizigo kushindwa kusafiri hivyo kutishia ajira na maisha ya watu wanaotegemea kuishi kwa kutegemea usafirishaji.
Makamu Mwenyekiti wa TAT, Omar Kiponza alisema tozo hiyo ya mizigo inayosafirishwa nje ya nchi imeleta changamoto kubwa kwa wadau wa usafirishaji kwani kuna magari zaidi ya 450 ya moja ya kampuni yaliyokuwa yakienda nchi ya nchi na mizigo wa mwezi yamefungiwa ndani bila kufanya safari zozote.
Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha (TAFFA), Stephen Ngatunga alisema ni muhimu kwa serikali kuangalia sheria hiyo ili iwe na manufaa kwa nchi badala ya kuwakandamiza wadau wa usafirishaji.
Alisema hivi sasa miziogo mingi imekuwa ikipishwa katika bandari za nchi jirani kwa kukwepa tozo hilo jambo ambali linaweza kuporomosha uchumi wa nchi unaotegemea sekta ya usafirishaji.
Alisema hivi sasa usafirishaji wa mizigo katika bandari ya Dar es Salaam umeanza kudorora kwa kiasi kikubwa na kuiomba serikali kuliangalia jambo hilo kwa makini ikiwa ni pamoja na kukutana na wadau wa usafirishaji ili kunusuru jambo hilo.
“Unajua kupitishwa kwa sheria hiyo kulifanyika haraka bila ya serikali kukutana na wadau wa usafirishaji ili kujua changamoto zao tunaomba tukutane na serikali ili kujadili jambo hili kwa kina kabla mambo hayajaharibika zaidi” alisema Ngatunga.