Wadau wa Sekta ya Barabara na Reli Watakiwa Kuchangamkia Fursa

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa(Wa pili kutoka kulia) akijadiliana na wadau wa miundombinu ya barabara na reli mara baada ya kufungua mkutano huo.Kulia kwake ni Katibu Mkuu Wizara wa Wizara hiyo (Sekta ya Ujenzi) Eng .Joseph Nyamhanga. Picha na Benjamin Sawe-Maelezo

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amewataka wadau wa sekta ya miundombinu ya Reli na Barabara kushirikiana na Serikali katika kuchangamkia fursa za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya sekta hiyo hapa nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Saba wa wadau wa Sekta hiyo, Prof. Mbarawa amesema kwa sasa Serikali kupitia Rais wa Awamu ya Tano inatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Tanga hadi nchini Uganda, ujenzi wa barabara ya kulipia wa Dar es Salaam-Chalinze KM 144 (Dar-Chalinze Express way) na ujenzi wa reli ya kati hivyo ni muhimu kwa wadau hao kutumia mkutano huo katika kuijadili miradi hiyo.

“Ni matumaini yangu katika mkutano huu mtajadili kwa pamoja namna ya kushirikiana na Serikali katika kutekeleza fursa za ujenzi wa miundombinu hapa nchini ikiwemo kuungana na Serikali (Public Private Partnership) au kwa njia nyingine yoyote,” amesema Waziri Mbarawa.

Aidha, Profesa Mbarawa amewataka wadau hao kutumia mkutano huo wa siku mbili kujadili namna bora ya kutunza na kuboresha miundombinu ya reli na barabara ili kuweza kudumu kwa muda mrefu. Amesisitiza wadau hao kuja kwa wingi nchini na kuwekeza katika sekta hiyo ili kupanua ushindani wa kibiashara katika soko la kitaifa na kimataifa.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akikagua ramani inayonyesha miundombinu ya barabara nchini wakati wa uzinduzi wa mkutano wa saba wa sekta ya Miundombinu ya barabara na reli, jijini Dar es salaam. Picha na Benjamin Sawe-Maelezo

Wazri Mbarawa amebainisha kuwa Serikali inaendelea kutafuta pesa kutoka kwa wadau mbalimbali na kushirikisha taasisi binafsi kupitia mpango wa kushirikiana baina ya Serikali na Taasisi hizo (Public Private Partnership) ili kutekeleza miradi ya miundombinu ya reli na barabara nchini.

Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) Eng. Bruno Ching’andu amesema kuwa licha ya TAZARA kuwa na treni za umma zinazotoa huduma za usafiri nchini bado inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uhaba wa fedha katika uendeshaji wa shirika hilo ikiwemo gharama za ujenzi na ukararabati wa mabehewa.

Mkutano huo wa siku mbili umewakutanisha wadau wa miundombinu ya barabara na Reli kutoka Taasisi za Serikali na wadau mbalimbali wa sekta hiyo kutoka ndani na nje ya nchi lengo likiwa ni kujadili kwa pamoja namna ya kuboresha miundombinu hiyo.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.