Katibu Mkuu wa baraza la Michezo Tanzania (BMT) Mohamed Kiganja amekutana na wadau wa Michezo Mkoani hapa na kukuta Lundo la lawama zikielekezwa kwa Viongozi wa Michezo mbalimbali
Kiganja alikutana na viongozi wa Michezo yote Mkoani hapa pamoja na wadau katika kituo cha michezo kanda ya Kaskazini kilichopo ndani ya uwanja wa Sheikh Amri Abeid na kuwaelezea juu ya kuendeleza michezo
“Kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha anafanya kitu ili kusaidia michezo kukua na kusonga mbele bila kuangalia serikali ifanye peke yake au kuviachia vyama vya michezo kwa kisingizio wao ndio walengwa” alisema Kiganja.
Kiganja aliongeza kuwa kila mtu anahitaji ajue haki zake na kulalamika bila kuwa na sababu ya msingi haitasaidia na mwisho itaongeza migogoro hivyo sio vyema kukaa kimya wakati michezo inashuka kutokana na uzembe wa watu wachache
Wadau walipopewa nafasi ya kuongea, walimwambia katibu huyo kuwa ligi ya mkoa iliyomalizika mwezi uliopita haikufuatwa utaratibu na iliendeshwa kwa ubabe na uongozi
Pia walienda mbali na kumwomba katibu huyo avunje uhalali wa bingwa wa Mkoa ambaye ni Timu ya Pepsi kwa madai ya kuwa kuna dalili ya rushwa ilitumika juu ya kumpata bingwa ambaye hakustahili
Hata hivyo Kiganja aliwajia juu wadau hao kwa kutoihusisha serikali katika masuala ya michezo na mwisho kukimbilia kutoa mashtaka hata sehemu isiyostahili kwa kuwa kila jambo lina sehemu yake