Na Mwandihi Wetu, Arusha
WADAU zaidi ya 500 wa utafutaji na uvunaji wa madini, Gesi asilia na Mafuta kutoka duniani kote, leo wanakutana Jijini Arusha kwenye kongamano linalotarajiwa kutumika kutangaza utajiri wa Tanzania kwenye sekta hizo muhimu kiuchumi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Kamishina wa Madini katika Wazira ya Nishati na Madini, Ally Samaje alisema kuwa kongamano hilo la siku tatu pia litaambatana na maonesho ya makampuni makubwa ya
utafiti na uchimbaji wa madini, gesi asilia na mafuta kutoka nchi mbalimbali.
Alisema pamoja na kuonyesha bidhaa na utalaamu wao katika sekta hiyo, wachimbaji na wafanyabiashara hao wakubwa pia watakutana na kubadilishana ujuzi na uzoefu na wachimbaji wadogo na wajasiriamali kutoka mikoa yote nchini.
“Pamoja na wataalamu wa sekta ya madini, gedi na mafuta, kongamano hilo la kwanza kufanyika nchini pia litaandamana na utoaji wa mada mbalimbali zitakazobainisha utajiri na fursa zilizopo nchini,” alisema Samaje.
Kwa mujibu wa Kamishina huyo, mada zingine zitahusu sekta ya usafirishaji, mawasiliano, miundombinu na ujenzi ambayo huenda sambamba na maendeleo ya sekta ya madini. Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli na mwenzake wa Mawasiliano na Uchukuzi, Dk. Harison Mwakyembe ni miongoni wa watu wanaotarajiwa kutoa mada kuhusu sekta zinazohusiana na wizara zao.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ndiye atakuwa mgeni rasmi katika sherehe za ufunguzi wa kongamano hilo ambalo miaka mingi imekuwa ikifanyika Cape Town, Afrika Kusini.