Wadau Anuwai Wakutana Kuijadili Elimu EAC

Nembo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki

Nembo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki

Na Mtuwa Salira, EANA-Arusha

WASOMI wabobevu, watawala, watafiti na waandaaji sera wanakutana mjini Arusha, Tanzania kuanzia Mei 5, 2014 kubadilishana uzoefu juu ya changamoto zinazoikabili sekta ya elimu na mfumo wake katika kanda ya Afrika Mashariki.

Mkutano wa tatu wa Taasisi ya Ubora wa Elimu ya Juu Afrika Mashariki (EAQAN) utafanyikia katika hoteli ya kitalii ya Ngurdoto, nje kidogo ya mji wa Arusha kwa kauli mbiu isemayo ‘’Ujenzi wa Utamaduni wa Ubora katika Sekta ya Elimu ya Juu Afrika Mashariki.’’

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Baraza la Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (IUCEA), Wilhelmina Balyagati, mkutano huo utatoa nafasi maalum kwa wataalamu hao kubadilisina uzoefu wa masuala ya kuzingatia ubora wa elimu, mifumo na changamoto zake.

Katika taarifa yake alifafanua kwamba lengo kuu la mkutano huo ni pamoja na kutoa nafasi kwa wanataaluma na wadau wa sekta wa elimu katika suala la ubora wa elimu, kuimarisha ushirikiano na mshikamano katika masuala mazima ya kuhakikisha ubora wa elimu katika kanda hiyo.

“Watajadili pia sera zinazohusu ubora wa elimu katika mfumo wa Elimu ya Juu ya Afrika Mashaiki na utendaji wake juu ya ubora wa elimu na kuchukua uzoefu bora zaidi unaoifaa kanda hii toka ndani na nje ya Afrika Mashariki,’’ aliongeza afisa huyo.

Jumla ya mada tatu kuu zitawasilishwa katika mkutano huo. Mada hizo ni pamoja na ushirikiano wa kimataifa katika kuoanisha mfumo wa elimu ya juu wa Afrika Mashariki, changamoto katika masuala mbalimbali ya elimu na jukumu la kusimamia ubora wa elimu katika Afrika Mashariki.