Na Baltazar Mashaka, TheHabari, MWANZA.
BAADHI ya wachambuaji wa pamba mkoani hapa wametishia kugoma kununua pamba kupinga kukatwa shilingi 100 kwa ajili ya kuchangia Mfuko wa Wakfu wa Kuendeleza zao la Pamba nchini (CDTF).
Wafanyabiashara hao pia wamepinga wakulima kukatwa kiasi kama hicho cha fedha kuchangia mfuko huo kwa madai kwamba, hauwasaidii kikamilifu wakulima wa pamba kupata madawa ya kuulia wadudu bali unanufaisha watu wachache.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana jijini Mwanza, wachambuaji hao wamemuomba Waziri Mkuu Mizengo Pinda aingilie kati suala hilo na kwamba, wako tayari kugawa mbegu bure kwa wakulima, si kuchangia mfuko huo.
Mmoja wa wachambuaji hao kati ya wanane amabye hakutaka jina lake litajwe gazetini aliliambia Uhuru kwamba, jana walikutana dharula katika Hoteli Vizano jijini hapa na kutoa maamzi ya kumtaka Pinda aingilie kati vinginevyo hawatanunua zao hilo.
“Kama tutanunua basi itabidi tuwalipe wakulima shilingi 900 badala ya bei elekezi ya shilingi 1100/= iliyotangazwa na Bodi ya Pamba kwenye Mkunatano wa Nane wa Sekta Ndogo ya Pamba uliofaanyika Juni 11 mwaka huu Mwanza.
Pamoja na maazimio mengine yaliyofikiwa na Mkutano huo uliohudhuriwa na Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Profesa Jumaane Maghembe, iliazimiwa wachambuaji na wakulima wakatwe shilingi 100 kwa kila kilo ya pamba kwa ajili ya kuchangia mfuko wa CDTF.
Kiasi hicho kitakatwa kuanzia msimu wa mwaka huu unaotarajiwa kuanza Juni 20 tofauti na misimu iliyopita ambayo wakulima na wachambuaji walikuwa wakikatwa shilingi shilingi 30 katika kila kilo moja.
“Baadhi yetu tumekutana na kujadili kwa kina, kwakweli hatuko tayali kuchangia mfuko huo, unanufaisha watu wachache tu wakati wakulima wanahangaika kila mwaka kupata madawa, madawa yanaagizwa kidogo na CDTF lakin kwenye takwimu zao wanaonyesha wameagiza mengi ya kutosha.” Alilalamika.
Alidai kwamba, hali hiyo inawafan ya wakulima wakose madawa na kupata hasara kwa kuambulia mavuno kidogo hivyo kama Serikali inataka kuinua zao hilo na kumsaidia mkulima, ufutwe.
“Juzi kwenye mkutano wa Sekta Ndogo ya Pamba, hatukupewa nafasi ya kuchangia mawazo yetu ndiyo maana tumekutana na kuweka msimamo huo, waliopewa nafasi ni viongozi wa serikali tu lakini tuna taarifa kuwa vigogo wa CDTF walifanya kampeni za kupitisha kiasi hicho ili wapate hela nyingi mwaka huu.” Alidai mchambuzi huyo.
Alieleza kuwa, wako tayari kugawa mbegu bure kwa wakulima kwa ajili ya msimu ujao wa 2011/2012 ili wao na wakulima wasikatwe kiasi hicho vinginevyo zao hilo litaendelea kudidimia.
Kwa mujibu wa Bodi ya Pamba katika Mkutano huo wa Nane, kiasi cha tani Milioni 300 zinakadiliwa kuvunwa katika msimu wa mwaka huu hivyo mfuko wa CDTF unatarajia kupata shilingi Bilioni 6o kutokana na makato hayo ya shilingi 200 kutoka kwa wachammbauji na wakulima baada ya kuuza kilo milioni 300 za pamba.
MWISHO.