*Wabunge wanawake nao wawachakaza Wawakilishi netibali
Na Joachim Mushi
TIMU ya mpira wa miguu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano ya Tanzania leo imeiadhibu bila huruma Timu ya mpira wa miguu ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar (BLW) baada ya kuichapa mabao 4 kwa 1.
Timu ya Bunge ambayo iliongozwa na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja (Mb) akicheza nafasi ya mlinzi wa kati imeonekana kuizidi kila idara timu ya Wawakilishi kutoka Zanzibar hivyo kuishambulia takribani muda wote wa mchezo. Kwa ushindi huo wabunge wamenyakuwa kombe na medali za dhahabu, huku Wawakilishi wakiambulia medali za shaba.
Hadi timu zinakwenda mapumziko ya dakika 45 za kwanza tayari wambunge wa Tanzania walikuwa wakiongoza kwa mabao 2 kwa moja. Magoli yote ya timu ya bunge mawili ya kipindi cha kwanza yalifungwa na mshambuliaji hatari wa timu hiyo, Sadifa Juma Hamis (Mb).
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo washambuliaji wa timu ya bunge waliendelea kulisakama lango la wapinzani wao, huku wapinzani nao wakijitahidi kufanya mashambulizi ya kushtukiza.
Katika mchezo huo ambao umedhaminiwa na Kampuni ya Serengeti Breweries kupitia Bia yake ya Serengeti, Wabunge ndiyo walionekana kujipanga vizuri na iliwachukua dakika chache kabla ya kuongeza goli ya tatu lililofungwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima. Hata hivyo bahati iliendelea kuwa nzuri kwa wabunge ambapo walifanikiwa kupata goli la nne lililofungwa tena na mfungaji wa mabao mawili ya kwanza, Hamis.
Hivyo hadi mpira unamalizika timu ya Bunge la Tanzania ilijipatia mabao 4 huku Wawakilishi wakiambulia goli lilelile moja walilolipata kipindi cha kwanza cha mchezo huo lililowekwa kimyani na Abdulah Haji Ally (Mb). Mchezo huo uliohudhuriwa na mamia ya washabiki ulikuwa mkali kitendo ambacho kilifanya kilele za mashabiki za kushangilia zikisikika muda wote.
Wakati huo huo, katika mchezo wa netibali kati ya Timu ya Wabunge Wanawake wa Tanzania na ile ya Wawakilishi nao umefanyika huku wabunge wakiwachakaza vibaya Wawakilishi kwa mabao 27 kwa matano.
Hali ilikuwa mbaya kwa timu ya wawakilishi muda wote baada ya kuonekana wamezidiwa kiasi kikubwa hivyo kuruhusu mvua ya magoli kuinyeshea timu yao ya netibali.
Mchezaji aliyekuwa nyota na mwiba kwa wawakilishi ni Grace Kiwelu (Mb) ambaye alifunga mabao 15 pekeyake kati ya 27 ya ushindi kwa timu yake. Mabao mengine ya timu ya Bunge netibali yalifungwa na Justina Shauri magoli 8 pamoja na Mkiwa Kiwaga aliyepachika vikapu 4. Kwa ushindi huo na timu ya netibali ya Bunge imejinyakulia kombe pamoja na medali za dhahabu.