Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia akizungumza na wanahabari nje ya ukumbi wa Bunge, mjini Dodoma. Wabunge wa Kambi ya rasmi ya Upinzani Bungeni, leo wameibuka na mtindo wa aina yake ndani ya Ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mjini Dodoma
Baada ya kuamua kuziba midomo yao kwa kugundisha karatasi na plasta kisha kutoka nje ya ukumbi huo ikiwa ni adhima ya kueleza hisia zao za kutosikilizwa mapendekezo yao na Naibu Spika, Mh. Dkt. Tulia Ackson.
Hii ni wiki ya tatu mfululizo wabunge wa Ukawa wamekuwa wakitoka bungeni baada ya kutangaza kuwa hawatahudhuria vikao vyote vinavyoongozwa na Dk Tulia, kufuatia kukataa hoja ya kujadili sakata la kufukuzwa wanafunzi 7,800 wa stashahada maalumu ya sayansi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).
Wabunge hao wameeleza kuwa hawaridhishwi na uongozi wa wa Naibu Spika na sasa wanaendelea na vikao vyao nje ya Bunge.
Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi) James Mbatia amesema wameanza kutoka kwa kufunga midomo na karatasi kuambia dunia kuwa bajeti imejaa ghiriba na udanganyifu mwingi kwa Watanzania.
Amesema watakwenda kuwaambia wananchi na hata kama mikutano imezuiwa, Rais John Magufuli asitegemee kwamba watanyamaza.
“Harakati hizi tulizianza tukiwa Chuo Kikuu na Dk Magufuli nilikuwa naye japo alikuwa mbele yangu. Dk Ackson alikuwa shule ya msingi na tangu wakati huo, harakati zinaendelea,” amesema Mbatia.