Wabunge Wamuenguwa Waziri Mkuu Somalia, Mugabe Kuteuwa PM

Abdiweli Sheikh Ahmed

Abdiweli Sheikh Ahmed

WABUNGE wa Somali wameng’oa kwa kura ya kutokuwa na imani naye Waziri Mkuu wa taifa hilo, Abdiweli Sheikh Ahmed madarakani. Hii ni mara ya nne kwa kiongozi huyo kupigiwa kura za kutokuwa na imani dhidi yake baada ya majaribio ya awali kumalizika kwa ghasia.

Taarifa za ndani zinasema serikali ilikuwa imeelemewa uhasama baina ya kiongozi huyo na rais wa taifa hilo Hassan Sheikh Mohamud. Wanasema kuwa hali ya usalama ilikuwa imezorotoa kutokana na mvutano huo.

Abdiweli anakuwa ni Waziri Mkuu wa pili kuondolewa madarakani mwaka huu. Hata hivyo Marekani imeshutumu kitendo hicho cha kumng’oa kiongozi huyo wakidai hakikuzingatia maslahi ya raia wa Somali.

Wakati huo huo, Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe anatarajiwa kuhutubia maelfu ya wajumbe katika siku ya mwisho ya mkutano mkuu wa chama tawala cha ZANU-PF mjini Harare. Katika hotuba yake Mugabe anatarajiwa pia kutangaza nani atachukua nafasi ya Makamo wa Rais, Joice Mujuru, ambaye ametuhumiwa kufanya ufisadi.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema anayehisiwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo ni Waziri wa Sheria, Emmerson Mnangagwa, lakini baadhi ya watu wanasema Rais Mugabe huenda akamteua Mkewe, Grace, kuwa naibu wake. Makamo wa rais ndiye huenda akarithi uongozi kutoka kwa Mugabe ambaye ametimiza miaka 90.

-BBC