Wabunge wa Tanzania wanajipendelea-DOVUTWA

Na Mafikiri Ernest
Dar es Salaam

Mwenyekiti wa taifa wa UPDP, Fahmi Nassoro Dovutwa

CHAMA cha UPDP kimehoji uhalali wa kila mbunge kulipwa Sh 90 milioni kama mkopo kuwawezesha kununua magari binafsi ya shughuli za kibunge huku wafanyakazi wa kada nyingine za kitaalamu zaidi wakisahaulika katika mpango kama huo.
Katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari jana, Mwenyekiti wa taifa wa UPDP Fahmi Nassoro Dovutwa amesema uamuzi wa kuwalipa wabunge fedha hizo unakiuka katiba ya nchi kwa vile ni wa kibaguzi.
“Ibara ya 13(2) ya Katiba ya Tanzania inatamka wazi kuwa ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na mamlaka yoyote katika Jamhuri ya Muungano kuweka sharti lolote ambalo ni la ubaguzi ama wa dhahiri au kwa taathira yake,” alisema Dovutwa katika taarifa yake.
Alisema kwa Bunge kujitungia kipengele cha kujilipa masurufu ni uvunjaji wa katiba inayokataza ubaguzi. “Iwapo kuna umuhimu kwa wabunge kulipana masurufu hayo, basi sisi tunaona hata wafanyakazi wa kada nyingine kama madaktari, wahandisi, mahakimu nao wanastahili kupata malipo hayo,” aliongeza.
Alisema hata kama malipo hayo yangekuwa halali basi kiutaratibu yanapaswa kulipwa baada ya mtu kufanya kazi na sio kabla, kama ilivyotokea kwa wabunge.
Dovutwa ambaye alikuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia UPDP katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana, alisema iwapo Bunge linatunga sheria au linaweka utaratibu wowote wa aina hiyo ni sharti uhusishe wafanyakazi wengine pia, ili kuondoa dhana ya ubaguzi.
Alisema chama chake kitatangaza mgogoro na chama hicho iwapo fedha hizo hazitarudishwa. Hakufafanua.
Jumla ya Sh. 3.24 bilioniu zimelipwa kwa wabunge kama mkopo kwa ajili ya kununua magari binafsi huku kila mbunge akiwekewa kwenye akaunti yake Sh 90 milioni kwa madhumuni hayo.
Hata hivyo, Spika wa Bunge, Bibi Anne Makinda, alikaririwa hivi karibuni akisema kuwa mikopo hiyo itatolewa kwa wabunge wanaohitaji tu, na italipwa katika kipindi cha miaka mitano. Kwa kawaida wabunge hulipa asilimia 50 tu ya mikopo hiyo.
Katika hatua nyingine, UPDP imepinga mpango wa wabunge kuwekewa bima ya matibabu katika hospitali za kulipia huku kikihoji: “Wamegundua udhaifu gani kwenye hospitali za umma?”.
Taarifa ya chama hicho inawata wabunge kutibiwa katika hospitali za serikali kama wanavyotibiwa wananchi wengine ili watambue ubora au udhaifu wa hospitali hizo.
“Kwa nini wao (Wabunge) wanazikimbia hospitali na zahanati za serikali, na hasa zile za kata ambazo wao ndio wanahimiza zijengwe? Bila shaka wamegundua kwamba haziko kwenye kiwango kuzuri cha matibabu, ndio maana wanataka wakatiwe bima ili watibiwe kwenye hospitali za binafsi kwa gharama kubwa,” ilisema taarifa hiyo.
“Huu ni udhaifu mkubwa sana katika utendaji. Kwani wabunge nao si binadamu kama walivyo wananchi wengine? Iwapo wanaona hospitali na zahanati za kata haziwafai, iweje waone kuwa zinawafaa wapiga kura wao,” ilihoji taaarifa hiyo.
Wabunge wapatao 360 wamekatiwa bima ya afya inayotarajiwa kuanza kutumika kabla ya mwezi Juni mwaka huu.
Wakati huo huo, Chama cha UPDP mkoa wa Dar es Salaam kimeunda tume ya maafa ambayo itafanya uchunguzi kuhusu milipuko ya mabomu iliyotokea katika kambi ya jeshi ya Gongo la Mboto.
Taarifa ya Mwenyekiti wa Mkoa wa chama hicho, Rajabu Mrisho, imesema chama kitafanya ziara kwa wahanga wa mabomu na kufuatilia kwa karibu ahadi zote zilizotolewa na serikali kuhusu kupatiwa huduma na malipo ya fidia.
“Tumeona ni vema kufanya hivyo kutokana na milipuko ya kambi ya Mbagala ambapo waliopatwa na maafa walilipwa viwango kidogo kinyume cha sheria, na huku kundi kubwa likidhulumiwa,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Mwisho