Wabunge: Vigogo dawa za kulevya wakamatwe

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema

Wabunge jana walicharuka bungeni wakitaka vigogo wa dawa za kulevya wakamatwe na kufikishwa mahakamani kwani tatizo la dawa za kulevya limezidi kuwa kubwa sanjari na kuongezeka kwa vijana wanaotumia dawa hizo maarufu kama mateja.

Waliyasema hayo wakati wanachangia muswada wa Sheria ya marekebisho ya Sheria mbalimbali wa mwaka 2011, uliowasilishwa bungeni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema.

Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, alisema inashangaza kuona kiwango cha dawa za kulevya kinachoingia nchini kikizidi kuongezeka lakini idadi ya watuhumiwa ikipungua.

“Tukisema eti tatizo linakuwa kubwa kwasababu ya udhaifu wa sheria si kweli, sheria zipo tena kali lakini usimamizi na utekelezaji wa sheria ndio mbovu, serikali iseme kwanini dawa zinaingia kwa wingi sana lakini watuhumiwa hawapo,” alisema Mnyika.

Alisema serikali lazima itaje majina ya watuhumiwa wanaosafirisha dawa za kulevya kuja hapa nchini badala ya kuweka mafaili ya watu hao makabatini.

Mbunge wa Kalenga (CCM), Dk. William Mgimwa, alisema vigogo wanaohusika na kuingiza dawa za kulevya hawakamatwi hivyo aliomba jitihada za makusudi kutoka serikalini. Alisema hali hiyo inatokana na kuongezeka kwa mianya ya rushwa miongoni watendaji serikalini hivyo kushindwa kuwajibika kwenye nafasi zao.

Mbunge wa Mbulu (Chadema), Mustafa Akonay, alisema inashangaza kuona kesi za dawa za za kulevya zinapungua wakati kiwango cha dawa za kulevya kinazidi kuingia nchini.

Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini, alisema ingawa sheria kali zipo, lakini inashangaza kuona mateja wakiongezeka katika miji mbalimbali nchini.

CHANZO: NIPASHE