Wabunge Nchini Uganda Wanunuliwa ‘iPads’

Wabunge Nchini Uganda Wanunuliwa 'iPads'

Wabunge Nchini Uganda Wanunuliwa ‘iPads’

SERIKALI nchini Uganda imewanunulia kompyuta ya kisasa (iPads) wabunge wake wote ikiwa ni hatua ya kuboresha utendaji kazi hatua iliyolalamikiwa na baadhi ya wananchi na wanaharakati nchini humo.

Ofisa Mkuu wa Bunge nchini humo amesema vifaa hivyo vitawafanya wabunge kuwa makini wakati wa vikao vya bunge. Kamishna wa bunge Emmanuel Dombo amesema kuwa wabunge sasa wanaweza kupata stakabadhi zao rasmi wakati hata wakiwa nje ya ofisi zao au wakiwa safarini.

Pia alisema kuwa pesa walizonunulia iPad hizo zitasaidia kuepuka kutumia kiwango kikubwa cha karatasi na kupunguza gharama ya matumizi. Wabunge wote wa bunge la Uganda ambao idadi yao ni 375, wanunuliwa zilizogharimu kima cha dola laki tatu na sabini.

Wakosoaji wanahoji ikiwa wanasiasa wanajua hata kuzitumia tabiti hizo na kusema kuwa tayari wananchi wanalipa pesa nyingi sana kwa mishahara ya wabunge. Mwaka jana wabunge wa Uganda walipiga kura kutaka mishahara na marupurupu yao kuongezwa kwa asilimia arobaini.

Pia walipokea marupurupu ya zaidi ya dola 40,000 ili kujinunulia gari jipya. Mbunge wa Uganda kwa sasa hulipwa, dola elfu nane, ingawa nchi hiyo inakumbwa na matatizo ya kiuchumi.

Wananchi wanasema kuwa hatua hiyo ya Serikali ni kuharibu pesa za walipa kodi, ikizingatiwa kuwa wabunge hao wanalipwa mishahara ya juu ambayo inawawezesha kujinunulia vifaa hivyo wao wenyewe.