Wabunge EAC wataka vikwanzo vya biashara ving’olewe

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dk. Richard Sezibera

Na Mwandishi wa EANA, Arusha

BUNGE la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) limetoa changamoto kwa nchi tano wanachama wa jumuiya hiyo kuongeza kasi ya kuviondoa Vikwazo Visivyo vya Kodi (NTBs) ili kujenga mazingira bora ya biashara katika kanda hiyo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchukuzi, Biashara na Uwekezaji, Dk. James Ndahiro alidokez kwamba NTBs kwa kiasi kikubwa vimeleta mchango hasa katika upanuzi wa biashara katika kanda hiyo ya Afrika Mashariki.

‘’Suala la NTB limelazimisha kuwepo kwa mkakati wa maamuzi ya makusudi ya pamoja ya kutaka kuviondoa kabisa vikwazo hivyo,’’ alifafanua Ndahiro alipokuwa anawasilisha ripoti ya hivi karibuni ya warsha juu ya NTB wakati wa ufunguzi wa kikao cha Bunge hilo, Jumanne, mjini Arusha.

Hiki ni kikao cha tano cha Bunge hilo na cha mwisho kabla ya kuapishwa Bunge jipya Juni 5, 2012.

Mambo yaliyoanishwa katika ripoti hiyo ambayo ni vikwazo ni pamoja na msongamano katika utoaji vibali, vituo vya kupima uzito wa magari hususan ni katika makorida ya Kaskazini na Kati,kukosekana kwa mfumo wa kufuatilia mizigo na hivyo kukwamisha usafirishaji wa mizigo na rushwa ambayo inawakumba wengi katika vituo vya mipakani.

Maeneo mengine ambayo yanahitaji kuingiliwa kati ni pamoja na kodi iliyoanzishwa hivi karibuni ya dola 200 za Kimarekani (zaidi ya shilingi 350,000 za Tanzania) kwa madereva wa malori na makondakta wao wanapoingia nchi yoyote mwanachama na vizuizi vingi vya barabarani.

Wakati wa majadiliano juu ya hoja hiyo, Ndahiro alisema kwamba Baraza la Mawaziri linatakiwa kuwasilisha ripoti ya kila baada ya miezi mitatu kuhusu hali halisi ya utekelezaji wa NTBs.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la EAC, Musa Sirma alisema kwamba Baraza lake limeongeza juhudi mara dufu katika kusimamia masuala ya NTBs. ‘’Tumeshuhudia upunguzaji wa vizuizi vya barabarani katika Jamhuri ya Kenya, kutoka 37 hadi kufikia vitano wakati idadi kubwa ya vizuizi nchini Tanzania vipunguzwa karibu ya nusu kutoka 37 hadi 15,’’ Mwenyekiti huyo wa Baraza ambaye pia ni Waziri wa EAC wa Kenya alieleza.

Sirma alisema pia kwamba Baraza hilo la EAC limekubaliana kuweka mfumo wa kanda wa kufuatilia mizigo ifikapo Desemba, mwaka huu. Mpaka sasa ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pekee ambayo imeanza kutekeleza mfumo wa ufuatiliaji wa mizigo.

‘’Tunataka kufanya suala la NTBs kuwa historia iliyosahaulika ifikapo Desemba 2012,’’ Sirma aliliambia Bunge.

Waziri huyo pia alilihakikishia Bunge hilo kwamba Jumuiya inaelekea katika lengo la kuwa na ushuri mmoja wa forodha kama ilivyoelekezwa na kikao cha wakuu wa nchi za EAC Aprili, 2012.

Alisisitiza kwamba Baraza la Mawaziri litajifanyia tathmini lenyewe juu ya utekelezaji wa masuala hayo na kutoa taarifa kwa Bunge hilo.