Wabunge Dar wawakumbuka Wananchi wao!

Mbunge wa Jimbo la Ubungo (CHADEMA), John Mnyika na Katibu wa Wabunge wa Dar es Salaam.

*Wampinga Dk Magufuli kupandisha nauli vivuko
WABUNGE wa Mkoa wa Dar es Salaam wamepinga hatua ya Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi kupandisha gharama ya kivuko cha Kigamboni kwa asilimia 100 kwa wananchi na kudai hatua hiyo itawaathiri wapiga kura wao kiuchumi hasa wakazi wa Kigamboni.

Akizungumza na vyombo vya habari jana Dar es salaam, Katibu wa wabunge hao ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika amesema kauli ya Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli kusema watakaoshindwa kulipia gharama hizo waogelee ni kutowajali wananchi.

Ameongeza kuwa utaratibu uliotumika kuongeza gharama za kivuko si halali kutokana na waziri kutofuata utaratibu mzuri ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wananchi kwa kuwatumia wawakilishi wao.

Aidha Mnyika amefafanua kuwa kutokana na ongezeko hilo la nauli kutoka sh. 100 hadi sh. 200 kwa abiria, Sh. 800 hadi sh. 1,500 kwa magari madogo aina ya salon, sh. 1,000 hadi sh. 2,000 kwa magari aina ya Pick Up, sh. 3,500 kwa mabasi madogo (daladala), huku magari yenye uzito wa kuanzia tani tatu na nusu yakitozwa sh. 7,500 badala ya sh. 5,000 ni kupandisha gharama za maisha kwa wananchi wa Kigambaoni.

Mnyika amedai wamepokea kwa masikitiko kauli iliyotolewa na Waziri, Dk. Magufuli kuhusu kupanda kwa gharama ya kivuko pamoja na vyombo vingine vya usafiri. Wabunge hao wameiomba Serikali kutokana na ugumu wa maisha isimamishe tozo hizo mpya mara moja na zifikiriwe upya.

Amesema tatizo si kiwango cha tozo kupanda au kushuka bali ni usimamizi wa mapato yanayopatikana katika vivuko hivyo kwani kiasi kikubwa cha fedha hizo hupotea kwa njia ya ufisadi. Wameitaka Serikali kuangalia namna ya kudhibiti mapato kwani eneo hilo ndilo lenye matatizo.

Naye Mbunge wa Jimbo la Kigamboni, Dk. Faustino Andungulile amesema anaungana na wananchi wa jimbo lake kupinga viwango hivyo na kueleza kuwa maandalizi ya kupanda kwa nauli hayakuwashirikisha wananchi.

Kwa upande wao wananchi wanaokaa maeneo hayo wameiomba Serikali kupunguza viwango hivyo kwani ni vikubwa mno kutokana na gharama za maisha kwa sasa kupanda kwa kiasi kikubwa.

Hata hivyo, wakati Dk. Magufuli akitoa sababu za kupanda kwa viwango hivyo vilivyopanda nchi nzima juzi alidai sababu zilizochangia kupandisha bei ni pamoja na ongezeko la mishahara ya watumishi serikalini kwa zaidi ya asilimia 100 na gharama za uendeshaji vivuko hicho.