WABUNGE wanne wa Chadema, ambao waliachiwa na polisi kwa dhamana wamesimulia mateso waliyoyapata wakiwa rumande baada ya kukamatwa juzi. Vigogo hao; Mbunge wa Mpanda Mjini Said Amour Arfi, Tundu Lissu (Singida Mashariki), Mustapha Akunaay (Mbulu) na Joyce Mukya (Viti maalumu), walikamatwa juzi baada ya wao na wafuasi wa chama hicho kutawanywa kwa mabomu ya machozi na polisi kwenye Viwanja vya Soweto, Arusha.
Wabunge hao waliachiwa baada ya kujidhamini wenyewe huku watu wengine 65 waliokamatwa pamoja nao wakiachiwa baada ya kudhaminiwa. Wote wanatakiwa kuripoti kwenye kituo hicho Julai 22, mwaka huu na wataelezwa hatma ya suala hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Operesheni wa Polisi, Kamishna Paul Chagonja alisema jeshi lake linaendelea kuwasaka Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Arusha, Godbless Lema na kuwaonya kuwa wanatakiwa kujisalimisha mara moja.
Chagonja alisema Mbowe na Lema wanatafutwa kwa kosa la kufanya kusanyiko lisilo halali katika viwanja hivyo vya Soweto walipokuwa wakitaka kuomboleza vifo vya watu watatu; Judith Moshi, Ramadhan Juma na Amir Ally waliofariki dunia baada ya kuumizwa kutokana na mlipuko wa bomu, Jumamosi iliyopita. Pia aliwaamuru Mbowe na Lema kuwasilisha mara moja ushahidi wa kuwahusisha polisi na shambulio la bomu na kama hawana imani na Polisi, basi wawasilishe ushahidi wao kwa Rais Jakaya Kikwete.
Lissu
Lissu, ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alilalamikia kitendo cha polisi kumwagia maji ya kuwasha baada ya kumkamata.
“Walinimwagia maji ya kuwasha kwa mfululizo nikalazimika kulala chini kifudifudi huku nikiwa nimefunika macho kukwepa yasiingie maji. “Kuna askari walitaka kunipiga lakini niliokolewa na mwenzao mmoja aliyenikinga nisishambuliwe. Kwa kweli ilikuwa hali ya hatari,” alisema.
Alisema polisi hao waliomkamata walivunja miwani yake kwa makusudi akisema aliikabidhi kaunta ikiwa haijavunjika.
“Wakati naingia mahabusu nilikabidhi miwani yangu lakini ajabu wakati tukiachiwa ilikuwa imevunjika.” Alilalamikia hatua ya polisi kuwashambulia kwa mabomu, kuwamwagia maji ya kuwasha walipokuwa wakiwatawanya watu waliokusanyika Soweto akisema awali, waliwaruhusu.
“Kwa maoni yangu na maoni ya wenzangu, hakukuwa na sababu ya polisi kupiga mabomu, risasi na kumwagia watu maji ya kuwasha kwani ni wao ndiyo walituomba tubebe dhamana ya uongozi kwa kwenda kuwaomba wananchi waliokusanyika pale uwanjani kutawanyika,” alisema Lissu.
Alisema Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha (OCD), Gilles Mroto ndiye aliyewaruhusu kuzungumza na wananchi ili watawanyike baada ya viwanja hivyo kuzuiwa kutumika kwa shughuli ya kuaga miili ya waliopoteza maisha kwenye tukio la bomu.
Alisema pamoja na ruhusa hiyo, polisi waliwaruhusu Chadema kuchukua magari yao yenye vipaza sauti ili wavitumie kuwatawanya wananchi hao lakini ajabu polisi ikawapiga mabomu mara baada ya Arfi kuwataka wananchi watawanyike kwenda Hospitali ya Mount Meru kutoa heshima za mwisho kwa marehemu.
“Kama ule mkusanyiko haukuwa halali, kwa nini polisi haohao walikaa na wananchi wale tangu asubuhi na wakaturuhusu kuzungumza nao ili watawanyike?”
Alisema kisheria, mkusanyiko usio halali unastahili kusambaratishwa kwa mabomu baada ya polisi kutoa ilani kwa wahusika kutawanyika tofauti na juzi akisema hawakutoa ilani yoyote.
Akunaay
Akunaay alisema polisi wanapaswa kubadilisha mbinu za kukabiliana na watu wanaodhani wamevunja sheria badala ya kukimbilia kupiga mabomu na kufyatua risasi.
“Mabomu na risasi ni kukomaza watu na kuwafanya wazoee milipuko. Itafikia hatua wananchi watajenga usugu na kuanza kupambana na polisi,” alisema na kuongeza:
“Polisi baada ya kutukamata na kutuweka chini ya ulinzi walitupiga hadi tukiwa kituoni bila sababu yoyote. Nadhani askari wetu wanapaswa kuacha kumalizia hasira zao za magumu yao yanayowakabili kwa kuwapiga watuhumiwa.”
Mukya
Mukya amelalamikia kitendo cha polisi kukataa kumpa fursa ya kumnyonyesha mtoto wake mchanga akisema malaika huyo alilazimika kushinda njaa kutwa nzima ya juzi na usiku kucha.
“Niliwaomba polisi wanikubalie kujidhamini au wanisindikize nikamnyonyeshe mtoto lakini walinikatalia kama vile ninakabiliwa na kesi ya mauaji,” alisema Mukya.
Akizungumzia suala hilo, Mwenyeki wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Susan Lyimo alisema: “Ni kinyume cha taratibu za haki za binadamu kwa mwanamke kunyimwa nafasi ya kunyonyesha mtoto wake.”
Polisi wajibu
Akizungumzia malalamiko ya wabunge hao, Kamishna Chagonja alisema hakuna mtuhumiwa ambaye anaweza kutoka mahabusu akaimwagia sifa kwa sababu siyo mahali pa kusifiwa, bali ni mahali penye kizuizi cha muda ili kuwezesha mkondo wa sheria kuchukua nafasi yake.
“Hatuna (polisi), roho ya Adolph Hitler (dikteta wa zamani wa Ujerumani), tupo kwa ajili ya kulinda wananchi na mali zao,” alisema.
Aidha, alikanusha madai ya Mukya ya kunyimwa ruhusa ya kumnyonyesha mwanaye akisema: “Siku hizi kuna dawati la jinsia katika vituo vyetu vya polisi kwa hiyo kama ni kunyonyesha lazima wangesimamia utaratibu wa kumwezesha kufanya hivyo, siyo kweli kwamba amekataliwa, haya ni maneno ya kulichafua jeshi.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema wanaojihusisha na uhalifu wowote huwa na imani kuwa watafanikiwa kujificha au kukwepa mkono wa dola na inapotokea wamekamatwa na kuchukuliwa hatua, huanza kujitetea kwa kuwashushia lawama polisi.
“Hasa wanasiasa na wanaharakati wakikamatwa na kuwekwa rumande, wengi hutoa manung’uniko mengi yakiwamo ya uongo, ilimradi kuchafua polisi mbele ya wananchi. Hatupo kwa ajili ya kusifiwa, bali kutimiza wajibu wetu,” alisema Sabas.
Kifo chaongezeka
Idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na mlipuko huo imefikia wanne baada ya mtoto Fahad Jamal (7), aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Seliani kufariki dunia jana. Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Paul Kisanga alithibitisha jana kufariki kwa majeruhi huyo aliyekuwa ameumia kichwani na kulazwa kwenye chumba cha wagonjwa wenye kuhitaji uangalizi maalumu (ICU).
Mmoja kuagwa leo
Kiongozi wa Chadema, Judith Moshi aliyefariki kwenye tukio hilo la bomu, leo anatarajiwa kuagwa kwa heshima zote za chama hicho katika moja ya makanisa jijini Arusha baada ya polisi kukizuia chama hicho kuendesha shughuli hiyo katika eneo la wazi.
Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Chadema, John Mnyika alisema baada ya kuagwa, marehemu Moshi atazikwa Arusha badala ya kusafirishwa kwenda mkoani Kilimanjaro kama ilivyokuwa imepangwa awali ili kutoa fursa kwa wananchi wa jiji hilo kushiriki katika mazishi yake.
“Kanisa gani na makaburi yapi tutamuagia na kumzika marehemu, tutatangaza baadaye au kesho asubuhi baada ya mashauriano kati ya viongozi na ndugu wa marehemu ambaye atazikwa kwa heshima zote za chama,” alisema Mnyika.
Awali, marehemu Moshi alitarajiwa kuagwa kwenye Viwanja vya Soweto kabla ya kusafirishwa kwenda Kilimanjaro lakini Jeshi la Polisi lilizuia shughuli hiyo kufanyika kwenye viwanja hivyo baada ya kupokea maelekezo kutoka kwa wamiliki wake ambao ni Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
CHANZO: www.mwananchi.co.tz