CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeanza kumeguka baada ya baadhi ya wabunge wake ambao ni Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, kuunga mkono kauli ya Naibu Katibu Mkuu wake, Mwigulu Nchemba. Nchemba ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha, Jumanne iliyopita akichangia wakati wa mjadala wa mabadiliko ya kanuni, alilitaka Bunge Maalumu la Katiba lijitathmini kama lina ulazima wa kuendelea wakati hakuna uhakika wa kupatikana kwa theluthi mbili.
Alisema kitendo cha Bunge hilo kukaa kwa siku 84 bila uhakika wa kupatikana kwa theluthi mbili kwa pande zote mbili inayohitajika kupitisha Rasimu ya Katiba Mpya, hakiwezi kueleweka kwa Watanzania.
Nchemba alisema ni vyema kujua idadi ya wanaoshiriki awamu ya pili ya Bunge hilo ili kutoa uthibitisho kimahesabu kama uamuzi wa kuendelea kwa Bunge unaweza kuwa na maana.
Jana Mwigulu Nchemba alizidi kusisitiza kauli aliyoitoa akisema ni msimamo wake binafsi kama mtoto wa maskini. Alisema anatambua jinsi walipa kodi watakavyoumia, rasimu hiyo itakapokwama kupita kutokana na kukosekana kwa theluthi mbili ya pande zote.
Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye juzi alijibu akisema kauli ya Nchemba ni mtazamo wake binafsi na hakuongea kama kiongozi wa chama hicho. Lakini jana wabunge mbalimbali wa CCM walijitokeza hadharani wakisema wanaunga mkono kauli ya Nchemba ili hesabu ijulikane badala ya kuendelea kutafuna fedha za wananchi bila tija.
Ali Keissy
Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Keissy, alisema msimamo wa Nchemba ndiyo msimamo sahihi ambao unapaswa kufuatwa kuliko kuendelea na Bunge wakati wakijua kuwa theluthi mbili haitapatikana.
“Kama kuna wabunge wa CCM wanaounga mkono kauli ya Mwigulu kwa asilimia 100 basi mimi naunga mkono kwa asilimia 500 na wako wabunge wengi tu wa CCM wanaunga mkono,” alisema.
Lembeli
Mbunge wa Kahama, James Lembeli aliliambia gazeti hili jana kuwa alichokisema Nchemba ni ukweli ambao haupingiki.
“Nakubaliana na Mwigulu kwa asilimia 100. Dunia ya leo siyo ya jana. Hii Tanzania ni ya wote, hata wajumbe wanaobeza mle ndani wajue wao wako wachache kuliko umma wa Watanzania,”alisema.
Lembeli alisema anaunga mkono kauli ya Nchemba ya kutaka hesabu ijulikane mapema kuliko kuendelea na Bunge wakati wakifahamu theluthi mbili haitapatikana na pia Katiba ni jambo la maridhiano.
Esther Bulaya
Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya alisema: “Kiukweli kutoka moyoni mwangu namuunga mkono Mwigulu Nchemba. Tusijisahau, sisi ndiyo tumepewa dhamana ya kulinda umoja wa kitaifa”.
Bulaya aliongeza kusema: “Katiba ni maridhiano, huwezi kuwapuuza wanasiasa ambao wakienda kwenye mikutano ya hadhara wanapata watu kama sisi. Tunatakiwa kuhakikisha taifa hili halichafuki”.
Mbunge huyo alisema kusitishwa kwa vikao vya Bunge Maalumu la Katiba haitatafsiriwa ni ushindi kwa kundi lolote, iwe ni Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), au CCM, ambao ni wengi.
“Sisi kuendelea na Bunge siyo ushindi wala Ukawa na wengine kutoka nje siyo ushindi. Sote tunapaswa kuwa na dhamira ya kweli ya kupata katiba itakayokubalika na wote,” alisema Bulaya.
Mwigulu
Akizungumza na Mwananchi jana kwa njia ya simu, Mwigulu Nchemba ambaye ni Mbunge wa Iramba Magharibi, alisema anatambua pia kuwepo kwa wajumbe wengi wa Bunge hilo kutoka CCM wanaomuunga mkono, ingawa bado hawajapata nafasi ya kuzungumza. Alisema wajumbe hao pia hawakubaliani na kitendo cha Bunge hilo kukaa kwa siku 90 bila uhakika wa kupatikana kwa theluthi mbili kwa pande zote mbili inayohitajika kupitisha rasimu.
“Kwa nini tukae sijui siku 87 au 90 wakati tunajua kwamba upande wa pili haujakamilika ? Kwa mujibu wa sheria inatakiwa ridhaa ya theluthi mbili kila upande, hii itajenga chuki hata kwa wananchi ambao wanaamini kwamba Katiba Mpya itapatikana kwa sababu tutakuwa tumekwama kutimiza malengo yaliyokusudiwa,” alisema Nchemba.
Alisisitiza kwamba yeye kama mtoto wa maskini ambaye amesomeshwa kwa kodi za walalahoi anajisikia vibaya kama Bunge hilo litaendelea na vikao wakati hawajajiridhisha kama theluthi mbili zitapatikana kupitisha rasimu hiyo. Pia ni jukumu lake kuishauri Serikali kwa nafasi yake ya Unaibu Waziri wa Fedha.
“Mimi ninavyoamini, wananchi wengi wanahitaji Katiba Mpya hata wale walioko nje ya Bunge. Kwa hiyo tunachotakiwa ni kujiridhisha kama akidi itafikiwa, badala ya kutumia fedha za walipa kodi wakati hakuna uhakika wa rasimu kupita,” alisema.
Alitumia fursa hiyo kuwasisitiza wajumbe wa Bunge hilo wanaounda kundi la Ukawa kurejea bungeni na kushiriki katika kuichambua rasimu hiyo katika masuala wanayokubaliana, yakiwamo; nishati, ufugaji na ugawaji wa pato la taifa.
Alisema kwa namna moja, ni vyema kujua idadi halisi ya wale wanaoshiriki katika awamu ya pili ya Bunge hilo na wale wasioshiriki, ili kutoa uthibitisho wa kihesabu kwamba uamuzi wa kuendelea kwa Bunge unaweza kuwa na maana.
Alisema iwapo hatua hiyo itashindikana, utetezi wa mwisho hautaweza kueleweka kwa sababu suala la kutimia kwa akidi kwa mujibu wa Katiba ni muhimu katika kufikia uamuzi na hasa kuangalia upya umuhimu wa kufikia maridhiano kwa sasa. Kwa upande wake Kangi Lugola, alipohojiwa na gazeti hili, alisema anatafuta fursa nzuri ya kuzungumzia jambo hilo hivi karibuni.
Malocha
Ignas Malocha, Mbunge wa Kwela , aliunga mkono hoja Mwigulu kwa asilimia 100 akihoji haraka ya nini kutegeneza Katiba ambayo haina maridhiano. Alisema haiwezekani wabunge walipwe Sh300,000 kwa siku kutunga Katiba ambayo haina maridhiano huku wananchi vijijini wakiishi bila majisafi, maabara, zahanati na wakati mwingine wakichangishwa kupata huduma hizo.
Alisema wabunge wa CCM hawataki Bunge liendelee, lakini wanakwama kufanya hivyo kwa sababu ya umaskini na kuiogopa CCM isije ikawawajibisha kama wataonyesha msimamo tofauti. Bunge la Katiba limepanga kutumia Sh20 bilioni huku wajumbe wake wakilipwa posho ya Sh300,000 kwa siku lakini hali halisi inaonyesha kwamba hata waketi siku 90 na watumie mabilioni yote hayo ya fedha, mwisho wa siku, theluthi mbili haitapatikana.
Uamuzi wa CCM kuamua kuendelea na vikao vya Bunge hilo unalalamikiwa na wananchi kuwa ni matumizi mabaya ya fedha za Watanzania maskini na wengine kumsihi Rais Jakaya Kikwete alivunje Bunge hilo mara moja. Kuendelea kwa Bunge hilo kunaonekana kuigawa nchi katika makundi yanayohasimiana, hali inayotafsiriwa kuwa hata kama katiba itapitishwa, itakuwa vigumu kupigiwa kura ya ndiyo.
CHANZO: Mwananchi