Wabunge CCM `Ndiyo`, Upinzani wasema `Hapana`

Bunge la Tanzania kwenye moja ya vikao vyake.

Baada ya Serikali kuongeza posho kwa wabunge, baadhi yao wametofautiana juu ya uamuzi huo huku wengine wakitaka Serikali iongeze posho kwa kada zote.

Hivi karibuni, vyombo vya habari viliripoti kuhusu nyongeza ya posho za vikao kwa wabunge kutoka Sh. 70,000 hadi Sh. 200,000 kwa kikao kimoja.

Wakizungumza na NIPASHE Jumapili kwa njia ya simu jana, wakati baadhi ya wabunge wa CCM wakionekana kukubaliana na uamuzi huo, wale wa upinzani wameendelea kushikilia msimamo wa kutaka posho zifutwe.

Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, alisema malipo ya posho hayana tija kwa kuwa kazi ya mbunge ni kuhudhuria vikao vya Bunge.

“Kama kazi ya Bunge ni kutunga sheria na kuisimamia serikali kwa kupitisha makadirio ya bajeti, mbunge hapaswi kulipwa kwa sababu ni kazi yake kuhudhuria vikao hivyo,” alisema.

Kutokana na hili, alisema malipo ya posho kwa namna yoyote ile sio halali, “hata kama itakuwa ni Sh. 10,000 sio halali.”

Kafulila alisema hakuna mantiki ya kulipwa kwa kukaa kwenye kikao ambacho ni wajibu wa kazi akieleza kwamba kumekuwa na ufujaji mkubwa wa fedha za umma kwa njia mbalimbali ikiwemo posho.

Alisema kazi ya Bunge ni kuhoji na kudhibiti ufujaji na wizi fedha za umma.

“Wananchi wasingelalamika kama tungekuwa tunatimiza wajibu wetu, Bunge linapaswa kusimama pamoja kuhoji ubadhirifu huu,” alisema.

Kwa upande wake, mbunge wa jimbo la Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe, alisema bado anatafakari kuhusu jambo hilo lakini anaishauri Serikali kutenda haki kwa ngazi zote.

Alisema kimsingi wabunge wanafanya kazi katika hali ngumu na gharama za maisha inazidi kupanda siku hadi siku, hali ambayo inawakabili wafanyakazi wa kada zote kwa sababu wanapokea mishahara midogo.

Filikunjombe alisema umefika wakati sasa kwa serikali kuwathamini watumishi wote wa umma bila kujali aina ya mtumishi wala kada yake.

“Ni kweli gharama za maisha zimepanda juu wakati mshahara ni mdogo, kitu muhimu ni Serikali kuangalia haki na sio kuchagua sehemu fulani,” alisema.

Hata hivyo alisema CCM ni chama kizuri chenye Sera na dira nzuri kwa wananchi, lakini kinaangushwa na utendaji mbovu wa serikali katika kutekeleza mambo mbalimbali iliyoahidi.

Naye mbunge wa Jimbo la Kilindi (CCM), Beatrice Shelukindo, alisema kwa kipindi hiki hakuna haja ya kuwachanganya wananchi kwa ongezeko hilo la posho na badala yake kuna mambo mazito yanayotakiwa kujadiliwa na kupatiwa ufumbuzi.

Alisema kiasi hicho cha pesa ni kidogo kulinganisha na wabunge wa nchi nyingine za jirani.

“Jamani tusianze kuwachanganya wananchi, hapa sijaona pesa za kulalamikiwa, kuna mambo mengi mazito ya kujadili na sio hili,” alisema Shellukindo.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI