Wapinzani wengine wa Young Africans, katika michuano ya kuwania Kombe la Shirikisho Barani Afrika, timu ya mpira wa miguu ya Medeama kutoka Ghana, itawasili Dar es Salaam, Tanzania Alhamisi Julai 14, 2016 kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (KQ), imefahamika.
Young Africans itaikaribisha Medeama ikiwa ni mchezo wa tatu kuwania taji hilo hatua ya makundi. Mchezo utafanyika saa 10.00 jioni Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Julai 16, mwaka huu.
Huu ni mchezo wa tatu kwa Young Africans katika harakati za kuwania Kombe la shirikisho hatua ya makundi. Michezo miwili ya awali ilikuwa ni dhidi ya Mo Bejaia ya Algeria ambako ilipoteza kwa bao 1-0 kabla ya kupoteza tena dhidi ya TP Mazembe, mechi iliyopigwa jijini Dar es Salaam.
Mchezo wa Jumamosi utachezeshwa na waamuzi kutoka Misri ambao ni Ibrahim Nour El Din atakayekuwa mwamuzi wa kati; akisaidiwa na Ayman Degaish na Samir Gamal Saad wakati mwamuzi wa akiba akiwa ni Mohamed Maarouf Eid Mansour.
Kamishna wa mchezo huo atakuwa Pasipononga Liwewe kutoka Zambia na maofisa wasimamizi ni Mfubusa Bernard ambaye atasimamia utendaji wa waamuzi wakati Mratibu Mkuu wa mchezo huo kutoka CAF atakuwa Ian Peter Keith Mc Leod.