OFISA wa ngazi ya juu katika Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya amani, Herve Ladsous amesema waasi wa M23 mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameanzisha serikali yao na kutoza watu ushuru. Mkuu huyo wa Umoja wa mataifa anayehusika na masuala ya usalama anasema waasi wa kundi la M23 wamejiundia serikali yao wenyewe mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Baada ya kukutana na wanachama wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu mgogoro wa nchi hiyo, Ladsous amewaambia waandishi wa habari kwamba kuna hali ya utulivu kiasi tangu wiki kama tano au sita zilizopita lakini hapana shaka hilo linaweza kubadilika haraka sana kuelekea pande zote.
Akizungumzia kitendo cha waasi kujitangazia serikali yao na kukusanya ushuru Naibu Gavana wa Jimbo la Kivu ya Kaskazini, Lutahichwa Mulwa Ale amesema ni jukumu la serikali kukomesha kitendo hicho na kuwasaidia wananchi wa mkoa wa Kivu ya Kaskazini.
Kundi la M23 likiongozwa na Bosco Ntaganda anayetakiwa na mahakama ya Kimataifa inayoshughulikia kesi za Uhalifu limeudhibiti mkoa wa Kivu ya Kaskazini karibu na mpaka wa nchi za Rwanda na Uganda.Wataalamu wa Umoja wa Mataifa pamoja na serikali ya Kongo wanaituhumu Rwanda kwamba inawaunga mkono waasi hao walioanzisha harakati zake za hujuma mwezi Aprili.
Rwanda lakini imekanusha tuhuma hizo hatua ambayo huenda ikachangia kuwakutanisha viongozi wa nchi hizo mbili katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa juu ya mgogoro huo wiki ijayo. Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wanaolinda amani wanatumia helikopta za kivita kuwasaidia wanajeshi wa serikali ya Kongo kuwatimua waasi hao wa M23 kutoka mji mkuu wa eneo hilo lenye utajiri wa rasilimali wa Goma.
Ladsous ambaye hivi karibuni alifanya ziara nchini Kongo Rwanda na Uganda amesema kundi hilo la waasi wamejiimarisha katika ngome yao kwenye mji wa Rutshuru ambako wameunda utawala wao mdogo wakidhibiti idadi ya watu pamoja na kukusanya kodi kwa watu wanaopitia kwenye eneo hilo jambo ambalo halikubaliki. Naibu Katibu Mkuu wa Un anayehusika na usalama Herve Ladsous
Ladsous ambaye ni naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa akihusika na usalama amesisitiza kwamba pande zote katika mzozo wa Kongo zinabidi kufanya kazi kwa pamoja kuelekea suluhisho la kudumu la kumaliza uhasama hasa ikizingatiwa kwamba ni muda mrefu sasa watu wanauwawa,wanateseka, kuachwa bila makaazi na wengi kuwa wakimbizi.
Aidha ametaka mamlaka ya Kongo iheshimiwe na kutoa mwito wa kuanzishwa tena juhudi ya kurejesha imani kati ya Kishasa na Kigali ambayo kutokana na uungaji mkono wa nchi za eneo hilo imekubali kupelekwa jeshi huru kulinda mipaka ya nchi hizo.
Huku kukiweko kiasi watu nusu milioni walioachwa bila makaazi kutokana na mapigano mapya mashariki ya Kongo shinikizo limeongezeka la kutaka hatua zichukuliwe katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa mjini New York mwezi Septemba kuhusu mgogoro huo.
-DW