CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) jana kimetoa mafunzo kwa wanahabari zaidi ya 30, ambao wanaandaliwa kwa lengo la kuripoti habari za unyanyasaji wa kijinsia (GBV) hapo baadae katika baadhi ya mikoa.
Wanahabari hao wamepata mafunzo hayo ikiwa ni hatua ya kuandaa kundi maalumu la wanahabari ambalo litakuwa likiripoti kwa kina habari dhidi ya vitendo vya kikatili kwa wanawake na wasichana ambao ndio waathiriwa wakubwa wa vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Akiwasilisha mada katika semina hiyo ya siku moja, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Ananilea Nkya amesema vyombo vya habari vimekuwa vikiandika mara kadhaa habari za GBV, lakini hali ya ukatili imeendelea kutokana na namna ya uandishi kukosa mtazamo wa kumaliza tatizo.
Amesema waandishi wa habari hawana budi kubadilika na kuweza kuandika habari za GBV kwa mtanzamo hasi wa kuleta mabadiliko katika jamii na hatimaye vitendo hivyo kukoma kama si kupungua.
“Lengo letu ni kuona wanahabari wanabadilika na kuandika habari zinazochangia vyombo au wahusika kuchukua hatua haraka na hivyo kuleta mabadiliko…,” alisema Nkya.
Mada nyingine katika semina hiyo iliwasilishwa na Mhariri wa dev.kisakuzi.com, Joachim Mushi, ambaye pamoja na mambo mengine aliwaelezea washiriki namna ya kuripoti habari za GBV katika mazingira anuai – ambazo zinaweza kuleta mabadiliko.
Washiriki hao wamepewa muda wa kuonesha uwezo walioupata katika semina hiyo juu ya kuripoti habari za unyanyasaji wa kijinsia kwenye vyombo vyao na baada ya hapo wanaofaa watatawanywa mikoani kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa habari hizo.