Na Mwandishi Wetu
WAANDISHI wa habari nchini Tanzania wanatarajia kuandamana mikoa yote kimyakimya ikiwa ni hatua ya kupinga kitendo cha mauaji ya mwandishi Daud Mwangosi (wa kituo cha Channel 10) kinachodaiwa kusababishwa na Jeshi la Polisi.
Waandishi wa Dar es Salaam wanatarajiwa kuanza maandamano yao katika Ofisi za Kituo cha Channel 10 jijini Dar es Salaam na kuandamana kimya kimya kwa amani kuelekea Viwanja vya Jangwani sehemu ambayo yatapokelewa maandamano hayo na kutolewa matamko mbalimbali kulaani kitendo hicho.
Akitoa taarifa leo jijini Dar es Salaam kuelezea maandamano hayo Katibu wa Jukwaa la Wahariri nchini Tanzania, Nevilli Meena alisema maandamano hayo yanafanyika ikiwa ni kuweka kumbukumbu kihistoria juu ya tukio lililotokea na kupinga vitendo vya kinyanyasaji wanavyofanyiwa wanahabari wanapokuwa katika majukumu yao.
Alisema maandamano hayo pia yanafanyika katika mikoa yote ya Tanzania kwa kuongozwa na viongozi wa Klabu za Wanahabari mikoa mbalimbali yakiwa na malengo sawa na waandamanaji watakuwa na mavazi ya rangi nyeusi kuomboleza msiba wa Mwangosi aliyeuwawa katika mapambano ya FFU na wanachama wa CHADEMA hivi karibuni mkoani Iringa.
Alisema tayari maandalizi yote ya maandamano hayo yamekamilika na Polisi wamekubali kutoa ulinzi kwa waandamanaji hadi kikomo cha maandamano, na kwa sasa hayata ishia Viwanja vya Mnazi Mmoja kama ilivyoelezwa awali kutokana na sababu ambazo alizitaja ni kutoelewana na viongozi wa Manispaa ya Ilala.
Mtandao huu utawaletea matukio ya maandamano hayo ‘live’ kuanzia awali hadi yanamalizika.