By James Gashumba,EANA-Arusha
SERIKALI za Afrika Mashariki na vyombo vya habari zinatakiwa kufanyakazi kama wadau, huku zikihakikisha kuendelea kuwapo kwa uhuru kwa kila upande katika utendaji wa majukumu yao.
Waandishi hao walitoa tamko hilo katika mkutano wa tano wa Vyombo ya Habari vya Afrika Mashariki ulionfanyika mjini Kigali, Rwanda ambapo pia waliwaomba wamiliki wa vyombo hivyo kutoa fursa za mafunzo kwa waandishi wao kuwawezesha kujiimarisha taaluma ili kuandika ipasavyo habari katika nchi tano wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
“…Tunataka vyombo vyetu vya habari kutoa habari za EAC kutoka kwenye muonekano wa EAC;kwa kuzingatia ukweli wetu badala ya kuegemea vyanzo vya habari za nje ambavyo vinaweza kuwa kinyume na malengo ya EAC,” yanasomeka maazimio yaliyotolewa mwishoni mwa mkutano huo wa siku mbili ambapo Shirika huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) lilibahatika kupata nakala zake.
Katika maazimio hayo ya vyombo vya habari Afrika Mashariki, hasa wahariri, wanatakiwa kuvipa kipaumbeke habari zinazoihusu EAC kwa kuvipa nafasi na muda unaohitajika kwenye vyombo vyao wanavyoviongoza.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame, Katibu Mkuu wa EAC ,Dk Richard Sezibera, Spika wa Bunge la EAC, Margret Zziwa, na mameneja wa vyombo vya habari, pamoja na wengine katika ukanda huo.
Pia mkutano huo uliwasihi wamiliki wa vyombo vya habari kubuni ushindani wa ndani utakaoibua majadiliano katika maswala mbalimbali juu ya jumuiya kushawishi uelewa kuhusu mtangamano wa EAC kwa upana.
‘’Mameneja wa vyombo vya habari wanawajibu wa kufuatilia na inapobidi kusimamia utoaji wa habari kwa kiwango kinachohitajika, ikiwemo ubora na usahihi,’’ walieleza.
Katika mkutano huo, waandishi hao na Rais Kagame walijadiliana namna ya kuanzia uhusiano baina ya vyombo vya habari na serikali ambapo Rais huyo aliwaambia waandishi hao “kusema habari zetu” badala ya kuviachia vyombo vya habari vya magharibi ambavyo mara kwa mara hupotosha ukweli.
Mkutano huo kwa pamoja uliamua kuanzisha Baraza la Habari la Afrika Mashariki kama chombo cha juu kitakachokuwa kinaratibu matumizi ya sheria na kanuni za habari katika EAC.
Katika kuhabarisha juu ya maswala ya jumuiya, Mkutano ulitoa changamoto kwa vyombo vya habari kuachana na matukio ya EAC na kubaini fursa na changamoto zitakazowanufaisha wakazi ndani ya jumuiya.
“Wakati mnafurahia uhuru wa habari, waandishi mnatakiwa kuongozwa na taaluma, usahihi na ulinganishi bila kuingilia haki za wasikilizaji wenu katika kupitisha maamuzi.”