Waamuzi, Kamishna waondolewa Ligi Kuu Vodacom

Moja ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Uwanja wa Taifa Dar es Salaam

Na Mwandishi Wetu

WAAMUZI watatu na kamishna mmoja wameondolewa kuchezesha na kusimamia mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kutokana na kuonesha upungufu katika uchezeshaji na usimamizi.

Uamuzi huo ulifanywa na Kamati ya Ligi iliyokutana Februari 11 mwaka huu ambapo pamoja na mambo mengine ilipitia taarifa za waamuzi na makamishna wa VPL ambayo Februari 12 mwaka huu inaendelea katika raundi ya 17.

Peter Mujaya wa Mwanza aliyechezesha mechi namba 101 kati ya JKT Ruvu Stars na Yanga amefungiwa kwa miezi 12 kwa mujibu wa Kanuni ya 26(a) ya Ligi Kuu ya Vodacom kwa kushindwa kumudu mchezo huo, hivyo kupata alama za chini.

Naye Isihaka Shirikisho wa Tanga ameondolewa kwenye orodha ya waamuzi wa VPL msimu huu kwa kushindwa kumudu mchezo namba 105 kati ya Simba na JKT Oljoro. Moja ya udhaifu alioonesha ni kushindwa kumuadhibu mchezaji Patrick Mafisango ambaye alimsukuma baada ya kumuonesha kadi nyekundu Haruna Moshi wa Simba.

Mwamuzi mwingine aliyefungiwa kwa miezi 12 kwa mujibu wa Kanuni ya 26(a) ni Kennedy Mapunda wa Dar es Salaam aliyechezesha mechi namba 107 kati ya Villa Squad na Simba. Moja ya udhaifu wa Mapunda ni kushindwa kumpa kadi nyekundu Fred Cosmas wa Villa Squad baada ya kumuonesha kadi ya pili ya njano.

Pia waamuzi wasaidizi Michael Mkongwa wa Iringa na Kudura Omary wa Tanga waliochezesha mechi namba 112 kati ya Yanga na Mtibwa Sugar wameondolewa katika mechi zilizobaki za VPL kwa kutokuwa makini. Mwamuzi wa mechi hiyo Ibrahim Kidiwa amepewa onyo.

Waamuzi wengine waliopewa onyo na kutakuwa kujirekebisha ni Hashim Abdallah wa Dar es Salaam aliyechezesha mechi namba 92 kati ya Moro United na Yanga, na mwamuzi msaidizi wa mechi ya Simba na Coastal Union, Issa Malimali wa Ruvuma.

Kamishna wa mechi namba 112 kati ya Yanga na Mtibwa Sugar, Mohamed Nyange ameondolewa katika orodha ya makamishna kwa mechi zilizobaki za VPL kutokana na ripoti yake kuwa na upungufu.