Frank Mvungi, MAELEZO
SHIRIKISHO la Vyuo Vikuu Chama Cha Mapinduzi (CCM) limempongeza Rais mteule wa Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli kwa kushinda kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu ulifanyika Oktoba 2015. Wamasema ushindi wa Dk. Magufuli ni kielelezo cha utendaji bora aliouonesha katika kuwatumikia Watanzania kwenye nyazifa alizotumikia kabla ya kuchaguliwa kwake.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa shirikisho la vyuo vikuu Chama cha Mapinduzi (CCM) Bi Zainab Abdallah wakati wa mkutano na waandishi wa Habari uliolenga kumpongeza Rais mteule kwa tiketi ya chama hicho.
“Akifafanua Bi. Zainab amesema kuwa Rais Mteule Dk. John Pombe Magufuli ameshinda kiti cha Urais kwa kuwa ndiye mtu pekee ambaye watanzania walikuwa wanamuhitaji ili aweze kuwaletea maendeleo kwa kuwa ni mchapa kazi na ameonyesha kwa vitendo dhamira hiyo katika utumishi wake kwa miaka yote iliyopita “alisisitiza Zainab Bi. Zainab amesema kuwa Rais mteule Dk. Magufuli anayo dhamira ya dhati yakuwaletea maendeleo watanzania ndiyo sababu hata kauli mbiu yake ililisisitiza kuwa “hapa kazi tu” hivyo ni wajibu wetu kama watanzania kusisitiza umoja na mshikamano na kuondoa tofauti zetu ili tufanye kazi kwa bidii ili kujenga uchumi wa taifa.
Akizungumzia wasifu wa Rais Mteule Dk. Magufuli; Bi Zainab amesema kuwa ni mtu mwenye uzalendo, mwadilifu, mchapa kazi, na ambaye watanzania wote wanamkubali kuwa anao uwezo wa kuliongoza Taifa katika kipindi hiki.
Kwa upande wa Uchaguzi mkuu Zainab amesema uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki hali iliyowapa nafasi watanzania kuchagua viongozi wanaowataka na kupelekea chama cha mapinduzi kuongoza katika uchaguzi huo kutokana na utendaji madhubuti wa viongozi wa Chama na Serikali.
Pia Bi Zainab alitoa wito kwa watanzania kudumisha amani na umoja wa Kitaifa ulioasisiwa na Viongozi wa kwanza wa Taifa hili ili kufikia maendeleo ya Kweli. Shirikisho la wanafunzi wa vyuo vikuu Chama cha Mapinduzi (CCM) limekuwa likihamasisha vijana kufanya kazi kwa bidii ili kujenga Taifa.