Vyuo Vikuu EAC Kurekebisha Mfumo wa Elimu

Mojawapo ya Jengo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Chuo hiki ni baadhi ya Vyuo Vikuu maarufu Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Mojawapo ya Jengo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Chuo hiki ni baadhi ya Vyuo Vikuu maarufu Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Na James Gashumba, EANA
 
BARAZA la Vyuo Vikuu la Afrika Mashariki (IUCEA) limenzisha mpango wa kufanyia mabadiliko makubwa mfumo wa elimu ya juu ili uzalishe wahitimu wenye ujuzi na sifa katika kanda kuweza kukabliana na mahitaji ya sasa ya kibiashara na ajira.
 
Mpango huo utawasilishwa katka mkutano wa siku mbili wa Wanataaluma na Mpango wa Ushirikiano wa Sekta ya Umma na Binafsi unaotarajiwa kufanyika mjini Kigali, Rwanda wiki hii. Mkutano huo na maonesho yameandaliwa kwa ushirikiano baina ya IUCEA, Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) na Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB).
 
Mpango huo wa mabadiliko ya mfumo wa elimu ya juu umejumuisha jukumu la kila mdau katika kurejesha hali mbaya inayozidi kuongezeka ya uzalishaji wa wahitimu wenye uwezo mdogo katika vyuo vikuu.
 
Katibu Mtendaji wa IUCEA, Prof. Mayunga Nkunya amethibitisha kuwepo kwa mkutano huo na kueleza kwamba hatua hiyo inafutaia utafiti uliofanywa na kubaini kwamba asilimia ipatayo 50 ya wahitimu wa vyuo vikuu hafai kwenye soko la ajira na hivyo kuongeza tatizo la ukosefu wa ajira.
 
“Tunawaleta pamoja wasomi na sekta binafsi ili kupanga mikakati ya kuwezesha kuzalisha wahitmu bora katika vyuo vikuu,” aliwaambia waandishi wa habari mjini Kigal mwishoni mwa wiki.
 
Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) lilishuhudia ripoti ya Baraza hilo ambayo pia imependekeza kwamba muundo wa elimu katika kanda hiyo hauna budi kuoanishwa katika ngazi zote za mitaala ya elimu ya juu kuruhusu wanafunzi kuweza kusoma katika chuo chochote katika kanda bila kujali ametoka nchi gani.
 
Mkutano huo utafanyika katika Hoteli ya Serena, Kigali kati ya Oktoba 23 na 24, 2014 chini ya kauli mbiu “Matumizi sahihi ya Uwezo wa Ubunifu Afrika Mashariki.”