Na Hassan Silayo – MAELEZO
15/3/2013 Vyombo vya habari nchini vimetakiwa kuwa mstari wa mbele kuwaelimisha na kuwasaidia wananchi kutambua na kujua kazi, muundo na majukumu ya Jeshi la Polisi ili kupunguza ukiukwaji wa haki za binadamu kwa baadhi ya Askari pale wanapotekeleza majukumu yao kazi.
Wito huo umetolewa leo na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Angellah Kairuki wakati wa uzinduzi wa kijitabu cha mambo 101 unayohitaji kuyafahamu kuhusu polisi lakini unaogopa kuyauliza uliofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora jijini Dar es Salaam.
Kijitabu hicho kiliandaliwa chini ya mradi wa kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki zao na kazi za polisi uliopo chini ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Ubalozi wa Uingereza nchini na Taasisi ya Jumuia ya Madola inayojishughulisha na masuala ya haki za binadamu yenye makao yake jijini New Delhi.
Waziri Kairuki alisema kuwa hivi sasa kuna haja kwa vyombo vya habari kuandaa vipindi vya redio na luninga ambavyo vitatoa elimu kwa umma na kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa muda mfupi haswa wale wanaoishi maeneo ya vijijini.
Aidha Waziri huyo pia alilitaka Jeshi la Polisi kutekeleza majukumu yao sawa sawa na sheria za Jeshi hilo na sheria ya mwenendo wa mashauri ya jinai,pamoja na sheria nyingine na kutotumia nguvu kubwa wakati wa ukamataji au kutuliza wa ghasia.
Kwa upande wake Naibu Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Julian Chandler alisema kuwa mradi huo ni moja kati ya miradi ambayo inatekelezwa na nchi yake kwa kushirikiana na taasisi na asasi mbalimbali za maendeleo.
Naye Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Jaji Kiongozi Mstaafu Amiri Manento alisema kuwa Jeshi la Polisi kukipitia kijitabu hicho litaelewa kitu gani wanatakiwa kufanya ikiwa ni njia moja wapo ya kuimarisha amani nchini.
Jaji Kiongozi Mstaafu Amiri Manento alisema kuwa ni muhimu Askari wakisome kijitabu hicho na kukielewa hata kama wanafahamu baadhi ya vitu,tunataka wananchi wajue haki zao za msingi.
Jumla ya nakala 4838 zimechapishwa kati ya hizo 4500 ni za kiswahili, 300 za kingereza na 38 za nukta nundu kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa macho, ambazo zitasambazwa bure kwa wananchi na taasisi mbalimbali katika mikoa ya ya Dar es Salaam,Zanzibar,Mwanza na Lindi na hapo baadae zitapelekwa katika mikoa mingine.