Na Mwandishi wetu
WAMILIKI wa vyombo vya Habari pamoja na Waandishi wa Habari hapa Nchini wameombwa kulipa umuhimu wa pekee zoezi la Sensa ya watu na makazi litakaloanza Agosti 26 katika maeneo mbalimbali kote nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mara John Tuppa alipokuwa akifungua mafunzo ya wiki mbili kwa wakufunzi 136 kutoka Wilaya zote za Mkoa wa mara watakaoendesha mafunzo kwa makarani na wasimamizi wa zoezi la uhesabuji wa sensa.
Amesema Vyombo vya Habari vinao umuhimu mkubwa sana katika kuhamasisha Wananchi katika kulipokea zoezi hilo na hatimaye kufanikisha malengo yaliokusudiwa na Serikali katika kupata takwimu sahihi na kuweza kupanga mipango madhubutio ya maendeleo.
Tuppa amesema kupitia Wahariri na Waandishi wa Habari katika vyombo mbalimbali wanayo nafasi kubwa ya kuwafanya Wananchi wakaelewa lengo la zoezi hilo ambalo Serikali imewekeza fedha nyingi ili kuhakikisha inapata takwimu sahihi ili kuweza kuharakisha maendeleo yanayokusudiwa kwa Wananchi wake.
Mkuu wa Mkoa wa Mara ameongeza kuwa Sensa ya mwaka huu inaumuhimu wake ili kuweza kufanikisha malengo ya melenia hivyo licha ya vyombo vya Habari pekee kufanya kazi za uhamasisha Taasisi nyingine zikwemo za dini,za Serikali na zile zisizo za Serikali zinapaswa kutoa ushirikiano ili kuweza kufanikisha zaidi.
“Umuhimu wa vyombo vya Habari unatambulika katika suala zima la uhamasishaji kwa kuwa asilimia kubwa ya Wananchi inakuwa inafatilia ikiwemo Redio,Tv pamoja na Magazeti lakini atupaswi kuwaachia peke yao kila mtu anahusika katika hili ili kafanikisha zoezi la Sensa ya watu na makazi ya Mwaka 2012”,alisema Tuppa.
Tuppa amewataka wakufunzi wa mafunzo hayo kuwa makini katika kufatilia mafunzo watakayokuwa wanapewa kwa muda huo wa wiki mbili na kuelewa kwa mapana yale watakayokuwa wanafunzwa na kuyazingatia ili baada ya hapo nao wakawafundishe makarani na wasimamizi wa zoezi la Sensa katika ngazi za kata na Tarafa.
Ameongeza kuwa wale waliteuliwa kupata mafunzo hayo wamepewa dhamana kubwa na Serekali katika kufanya kazi hiyo hawategemei kupokea visingizio vya aina yeyote kwa yule atakayevuruga zoezi hilo na ndicho kilichopelekea kuweka mkazo kukakikisha wanakuwa makini katika kufatilia mafunzo watakayokuwa wanapewa kwa muda wote.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa wa Mara amewataka Wananchi kutoa ushirikiano kwa makarani na wasimamizi katika muda wote wa zoezi hilo litapokuwa linaendelea na kuongeza kuwa tayari wamekwisha kuziagiza kamati za ulinzi katika ngazi zote kuhakikisha kunakuwa na ulinzi kwa Wananchi na vifaa vyote vitakavyohusika katika zoezi hilo.