Polisi, Wamachinga wakabiliwa, Kandoro asema mapambano ni magumu
JIJI la Mbeya jana liligeuka uwanja wa vita. Milio ya mabomu, risasi vilitawala sehemu kubwa ya jiji hilo na kusababisha watu kadhaa kujeruhiwa huku kituo kimoja cha polisi kikichomwa moto na magari kadhaa hali iliyosababisha huduma karibu zote kusimama kwa muda mrefu.Vurugu hizo zilitokana na operesheni iliyofanywa na askari wa Jiji la Mbeya ya kuwaondoa wafanyabiashara wadogo ‘Wamachinga’ katika Mtaa wa Makunguru, Mwanjelwa.
Katika vurugu hizo Kituo cha Polisi cha Nanenane kilichomwa moto na raia mmoja aliripotiwa kujeruhiwa kwa risasi mguuni huku barabara zote zinazoingia na kutoka katika jiji hilo zikifungwa. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro alisema: “Hali ni mbaya. Mapambano ni magumu,” akiwasihi wamachinga kuacha mapambano na badala yake wawasilishe kwake madai, hoja na malalamiko yao.
Mbali ya kufungwa kwa barabara hizo, wananchi walishindwa kutoka majumbani na wale waliokuwa maofisini walishindwa kurejea makwao kutokana na ghasia hizo ambazo zilikuwa kubwa zaidi katika maeneo ya Mwanjelwa, Kabwe, Soweto, Nanenane na Uyole ambako kote huko wamachinga walichoma moto matairi barabarani kuzuia magari na watu kutembea.
Vurugu hizo zilianzia Makunguru saa 1:30 asubuhi baada ya askari wa jiji kuwazuia wamachinga hao kupanga tena bidhaa zao kwenye eneo hilo. Ilielezwa kwamba wamachinga hao waliamua kupanga bidhaa zao hapo baada ya kuondolewa na kuahidiwa kupangiwa eneo jingine wiki moja iliyopita bila mafanikio.
Askari hao wa jiji walizidiwa nguvu na vijana hao waliokuwa wakitumia mawe ndipo jeshi la polisi lilipotaarifiwa na kufika katika eneo hilo wakiwa na bunduki, mabomu na magari maalumu yakiwemo ya maji ya kuwasha.
Licha ya kutumia zana hizo, wamachinga waliokuwa wakikimbia huko na huko wengine wakiwa wamevua mashati walikabiliana na polisi hao.Kadri muda ulivyosonga, ghasia hizo zilikuwa zikipamba moto kwani wamachinga hao walifunga barabara katika baadhi ya maeneo kwa mawe na magogo huku wengine wakipindua magari na kuyatumia kufunga barabara hizo.
Mashuhuda walisema katika baadhi ya maeneo polisi walionekana kuzidiwa nguvu na wamachinga hao kwani kila walipofika katika sehemu moja kuwatawanya, wengine waliibukia upande mwingine.
Wamachinga hao hawakujali mabomu ya machozi kwani kila yaliporushwa na polisi walijimwagia maji usoni na kuendelea kujibu mashambulizi kwa mawe. Wengine waliyawahi na kuwatupia tena polisi. Ilifikia mahali polisi nao wakaonekana kuishiwa mabomu hivyo baadhi ya maeneo walisikika wakirusha risasi za moto hewani kujaribu kuwatawanya wamachinga hao.
“Kila mmoja amebaki sehemu alipo kutokana na mji mzima kuzagaga vurugu,” alisema mkazi wa Ilemi, Bryson Mwakitalima na kuongeza kwamba baadhi ya wafanyabiashara walijifungia kwenye maduka yao huku wengine wakiyafunga na kutokomea. Inadaiwa kwamba baadhi ya wamachinga hao waliteka malori ya mafuta eneo la Uyole na kupora mafuta kwa madai ya kuyatumia kujihami ikiwa polisi wataendelea kuwanyanyasa.
Katika baadhi ya maeneo, wamachinga walisikika wakiimba nyimbo ambazo ujumbe wake mkubwa ulikuwa ni kuchoka kunyanyaswa. Mmoja wa wafanyabiashara hao, Hamis Ramadhani alisema wameamua kufanya hivyo ili kuileza Serikali kuwa wamechoshwa na manyanyaso wanayopata kutoka kwa askari wa jiji kuwaondoa katika maeneo wanayofanyia biashara.“Wanatutaka tuondoke hapa sasa twende wapi! Hakuna mahali ambako wametutengea nashangaa wanatung’ang’ania tuondoke na sisi hatukubali,” alisema.
Kandoro: Hali ni mbaya
Kandoro alilazimika kukatisha ziara yake ya siku tatu wilayani Mbozi kutokana na mgogoro huo. Alirejea jijini Mbeya jana na kuitisha kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa
“Hali ni mbaya. Mapambano ni magumu,” alisema Mkuu wa Mkoa kwa simu jana na kuthibitisha kuwa barabara nyingi zimefungwa na wamachinga hao.
Kandoro ambaye ni Mwenyekiti wa kamati hiyo ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya alisema wameweka mikakati kadhaa kuhakikisha hali ya amani inarudi. Miongoni mwa mikakati hiyo ni kutumia magari yenye vipaza sauti kuwatangazia wananchi kuwa watulivu na pia kuwatangazia wamachinga kuacha mapambano na kuwasilisha kwake matatizo yao ili ayatatue.
“Tunachowaambia ni kwamba kama kuna mtu ambaye ana hoja au malalamiko yoyote ayalete tujadiliane ili tuyapatie ufumbuzi,” alisema Kandoro.Mkuu huyo wa Mkoa alisema mgogoro huo umekuwa mgumu zaidi kutokana na kuchukua mrengo wa kisiasa.
Alisema kwenye vurugu hizo, bendera za CCM zinachomwa na kupandishwa za Chadema.Alisema hadi jana jioni, watu 127 walikuwa wamekamatwa kuhusiana na vurugu hizo. Habari hii imeandikwa na Brandy Nelson, Mbeya na Lauden Mwambona na Leon Bahati. Dar.
CHANZO: Mwananchi