*Yakabidhi madawati 225 kwa shule 5 za Ilala, Kinondoni
TATIZO la uhaba wa madawati kwa shule anuai za msingi nchini ambalo limekuwa kero kubwa na kuchangia baadhi ya wanafunzi kufanya vibaya kimasomo shuleni huenda likapata ufumbuzi kutoka na taasisi na mashirika binafsi nchini kuendelea kusaidia suala hilo.
Moja ya mashirika hayo ni mfuko wa kusaidia jamii wa kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania, ambao leo umekabidhi madawati 225 yenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 20, ikiwa ni utekelezaji wa muendelezo wa utoaji wa madawati katika shule za msingi za Mkoa wa Dar es Salaam.
Akizungumzia mradi huo Ofisa Mkuu wa Masoko na Uhusiano wa kampuni hiyo, Mwamvita Makamba amesema mradi huo ni sehemu ya kutambua umuhimu wa elimu kwa watoto wa Kitanzania kama nyenzo ya kuwajengea mazingira bora ya maisha yao ya baadaye na kulisadia taifa katika fani mbalimbali.
Vodacom Foundation imekuwa ikiweka mkazo kusaidia sekta ya elimu kama eneo muhimu la kuchangia nguvu na juhudi za serikali katika ustawi wa jamii nchini, hii ni awamu ya pili kwa mwaka huu na ni imani ya Vodacom kwamba madawati hayo yatapunguza uhaba katika shule ambazo zitaguswa.
“Tunatambua ukubwa wa tatizo na kwamba lipo takribani nchi nzima na tunaguswa nalo kama kampuni yenye kujali maisha ya watanzania na ndio maana kila mwaka tumekuwa tukiendesha kampeni maalum ya kuchangia madawati ni imani yetu kwamba ipo siku changamoto hii itabakia kuwa historia,” alisema Mwamvita.
Amesema ukosefu wa madawati nchini ni changamoto ambayo dhahiri ahitaji kufumbiwa macho wala kuzibiwa masikio inahitaji nguvu za pamoja za kila wadau ili kuwawezesha wanafunzi ambao ndio nguvu kazi ijayo ya taifa kuwa na mazingira bora, salama na kuwawezesha kufanya vema katika masomo yao.
“Inaumiza sana unapoona watoto wameketi sakafuni au kubanana katika dawati moja darasani, hii lazima itapunguza uwezo wao wa uelewa na ufuatiliaji masomo darasani ndio maana tukaamua kama kampuni inayoungwa mkono na watanzania kuonesha upendo wetu kwa kuwa na kampeni kabambe ya kusaidia madawati mashuleni,” Amesema Ofisa Mkuu wa Masoko na uhusiano wa Vodacom.
Awamu hii imenufaisha shule za msingi tano ambazo ni Maarifa shule ya Msingi (Ilala) Kombo shule ya Msingi (Ilala) Vingunguti Shule ya Msingi (Ilala) Mwongozo Shule ya Msingi (Kinondoni) Kimara B Shule ya Msingi (Kinondoni)