Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Simu za mkononi ‘Vodacom Tanzania’ imefikisha idadi ya wateja milioni 10, hivyo kuwa ni kampuni pekee ya simu yenye wateja wengi nchini. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) hivi karibuni inaonesha Vodacom inawateja milioni 10 ikifuatiwa na Kampuni ya Airtel yenye wateja 5,927,417.
Kampuni inayoshika nafasi ya tatu ni Tigo yenye wateja 4, 671, 263, ikifuatiwa na kampuni ya Zantel 1,354,098, TTCL kampuni ya simu kongwe kuliko imeshika nafasi ya tano kwa wateja 226,153, Sasatel 8,498 huku Benson ikishika mkia katika orodha hiyo kwa kuwa na wateja 2,074.
Wakizungumzia taarifa hiyo kampuni ya Vodacom imesema ina kila sababu ya kuendelea kuwashukuru wateja wake na Watanzania wote kwa jumla kwa uaminifu na mchango wao mkubwa wanaoendelea kuuonesha kipindi chote cha miaka 11 kwa kampuni hiyo.
“Mafanikio mbalimbali tuliyoyapata hadi hivi sasa ni matokeo ya kuelewa mahitaji muhimu ya wateja wetu na kuhakikisha kuwa tunayatimiza na kuwafanya wateja wetu waendelee kufurahia huduma zetu. Kama tulivyowaahidi wakati wa mabadiliko ya muonekano wetu, tunapenda kuwasisitizia kuwa tutaendelea kuyatimiza yale yote tuliyowaahidi na kuyaboresha zaidi,” inasema Vodacom katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.
Vodacom imesema itaendelea kuhakikisha kuwa inakuwa mtandao ulio bora na unaotoa huduma na bidhaa za bei nafuu zaidi nchini, ili kuwarahisishia huduma Watanzania na wateja wengine wa mtandao huo.