Vodacom yakamilisha Awamu ya Pili Ujenzi wa S/Msingi Ruvu Darajani

Haya ndiyo madarasa matatu ya Shule ya Msingi Ruvu Darajani iliyopo mkoani Pwani yaliyojengwa na Vodacom Foundation. Vodacom pia ilikabidhi madawati 100 kama msaada ambavyo kwa pamoja vimegharimu zaidi ya sh. milioni 98.


0fisa Mkuu wa Masoko na Mahusiano wa Vodacom Tanzania, Mwamvita Makamba, akikata utepe kuashiria uzinduzi wa vyumba vitatu vya madarasa pamoja na madawati 100 vilivyokabidhiwa rasmi na Vodacom Foundation kwa ajili ya Shule ya Msingi Ruvu Darajani iliyopo mkoani Pwani, msaada huo umegharimu zaidi ya sh. milioni 98. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Shule za Msingi Wilaya ya Bagamoyo na kushoto ni Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mary Nzowa.

*Yatoa pia madawati 100

KAMPUNI ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania imekabidhi vyumba vitatu vya madarasa pamoja na madawati 100 katika Shule ya Msingi Ruvu Darajani, Chalinze Mkoa wa Pwani ikiwa ni sehemu ya pili ya mradi wa kuiboresha shule hiyo unaofadhiliwa na Mfuko wa Kusaidia Jamii- Vodacom Foundation.

Madarasa hayo pamoja na madawati yamegharimu zaidi ya sh. milioni 90 zilizotolewa na Vodacom katika mwaka wa fedha wa 2011/12 kwa ajili ya mradi huo.

Akikabidhi madarasa hayo Ofisa Mkuu wa Masoko na Mahusiano wa Vodacom, Bi. Mwamvita Makamba amesema sekta ya elimu ni moja ya kipaumbele kikuu cha Vodacom kusaidia maendeleo ya wananchi, kuboresha vipato na kupunguza umasikini katika jamii pamoja na kuwajengea watoto msingi wa maisha bora ya baadae.

Ofisa Mkuu wa Masoko na Uhusiano wa Vodacom, Mwamvita Makamba na Mkurugenzi Mkuu wa Shule za Msingi Wilaya ya Bagamoyo, Phares Obadiah wakiteta jambo na baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Ruvu Darajani iliyopo mkoani Pwani mara walipofika shuleni hapo kukabidhi msaada wa madarasa matatu na madawati 100, msaada huo umegharimu zaidi ya milioni 98.


Mwaka 2010 Vodacom iliamua kuijenga upya shule hii baada ya kuguswa na uchakavu wa majengo yake ulioathiri utoaji wa taaluma huku ikiwa inahudumia mamia ya watoto wa eneo hili la Ruvu Darajani na maeneo jirani ambayo wengi wao ni wa kipato cha chini na cha wastani.

“Vodacom iliamua kujenga madarasa mapya na sio kuyakarabati ya zamani ili kutoathiri shughuli za masomo shuleni hapo ambapo wakati wote wa ujenzi masomo yamekuwa yakiendelea katika madarasa ya zamani na wanafunzi huhamia kwa awamu katika vyumba vipya vya madarasa kadri ujenzi unavyokamilika.” Alisema Mwamvita

Shule hiyo ya msingi ya Ruvu Darajani ilijengwa mwaka 1964 na haijawahi kufanyiwa ukarabati mkubwa hadi Vodacom kupitia mfuko wake wa Vodacom Foundation ilipoamua kuijenga upya katika mradi wa awamu tatu unaohusisha ujenzi wa vyumba tisa vya madarasa.

Ili kuhakikisha inatoa kitu kilichokamilika kukidhi mahitaji ya madarasa Vodacom Foundation imekabidhi pia madawati 100 yenye gharama ya sh. milioni 8.9.

“Vodacom ina namna nyingi yakutimiza azma yake ya dhati ya kubadili maisha ya watanzania. Leo tunapoangalia nyuma tunagundua jambo kwamba tumewajengea watoto wetu mazingira bora ya elimu yanayowawezesha kujenga msingi imara wa maisha yao ya baadae.” Alisema Mwamvita.

“Vodacom biashara ni sehemu moja ila namna tunavyoshiriki katika juhudi za kubadili maisha ya jamii ni sehemu nyingine muhimu inayotupatia ufahari wa kuwa katika biashara na kwa mantiki hiyo ndio maana Vodacom inawekeza kiasi kikubwa cha fedha kila mwaka kusaidia sekta ya elimu, afya, mazingira na michezo kwa masilahi ya jamii.” Aliongeza Mwamvita.