*Ni awamu ya pili kampeni ya madawati 1000
*Lengo kupunguza uhaba wa madawati s/msingi
IKIENDELEZA utamaduni wake wa kusaidia jamii kwa lengo la kubadili maisha mfuko wa kusaidia jamii wa kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom jana ulikabidhi madawati 250 ikiwa ni utekelezaji wa awamu ya pili ya kampeni ya utoaji wa madawati katika shule za msingi katika mkoa wa Dar es salaam yanayofikia madawati mia tano yenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 45.
Akikabidhi madawati hayo leo kwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni ambae anakaimu pia Ukuu wa Wilaya ya Temeke Bw. Jordan Rugimbana, Mkuu wa Mfuko wa Vodacom wa kusaidia jamii – Vodacom Foundation Yessaya Mwakifulefule amesema kampuni yake inatambua umuhimu wa elimu kwa watoto wa kitanzania kama amana muhimu ya kuwajengea mazingira ya maisha bora ya kujitegemea na pia kulisadia taifa.
“Inaumiza sana unapoona watoto wameketi sakafuni au kubanana katika dawati moja darasani, hii lazima itapunguza uwezo wao wa uelewa na ufuatiliaji masomo da ndio maana Vodacom kampuni inayoungwa mkono na watanzania zaidi ya milioni kumi ikaamua kuonesha upendo kwa kuwa na kampeni kamambe ya kusaidia madawati mashuleni.” Amesema Mkuu wa Vodacom Foundation.
Jumla ya madawati 1000 yenye thamani ya shilingi 89,000,000/= yatakuwa yametolewa na Vodacom kwa shule za msingi kati ya Aprili na Oktoba mwaka huu.