Na James Gashumba, EANA-Arusha
VIZUIZI visivyo vya Kodi (NTBs) vinaendelea kuwa vikwazo katika harakati za ufanyaji biashara kwenye nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kwa mujibu wa ripoti ya utafiti uliofanywa katika bandari za Mombasa, nchini Kenya na Dar es slaam nchini Tanzania.
Ripoti hiyo imefafanua kwamba ukiritimba wa utendaji katika bandari hizo mbili, vizuizi vya barabarani visivyo vya lazima na masuala ya utawala ni miongoni mwa vikwanzo katika uendeshajai biashara kwa ufanisi katika kanda hiyo ya EAC. Vituo vingi vya kupima uzito wa magari katika makorida ya Kaskazini na Kati, taarifa hiyo imeeleza, hufanya biashara zisifike kwenye maeneo husika kwa wakati.
Baadhi ya maeneo yanayoathiriwa na hali hiyo ni pamoja na Burundi, Rwanda na Uganda zikiwa na vituo 36 kati ya Mombasa na Kigali na vituo 30 kati ya Dar es Salaam na kwenye mpaka wa Rusumu, nchini Rwanda. Uganda nayo ina vituo tisa kati ya Malaba na Gatuna.
Nchi za Rwanda na Burundi ndizo zinazotambulika EAC kwamba zinafanya kila linaloweza kuondoa vizuizini vyote vya barabarani kuliko nchi nyingine tatu wananchama zilizobakia za Kenya, Uganda na Tanzania.
Ripoti hiyo inaeleza kwamba taratibu ndefu za kupata kibali cha kufanyakazi miongoni mwa nchi wanachama wa EAC, hususan ni Tanzania pia ni changamoto. Mambo mengine yaliyoripotiwa pia ni pamoja na ukosefu wa maeneo ya kuegesha magari katika maeneo ya mpakani, rushwa miongoni mwa makorida hayo mawili na pia kuzuiwa kwa magari kusafiri zaidi ya saa 12 jioni nchini Tanzania.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Viwanda wa Rwanda, Emmanuel Hategeka, aliuambia mkutano wa waandishi wa habari hivi karibuni mjini Kigali kwamba yapo majadiliano makali yanaendelea kuhakikisha kwamba vikwazo vyote hivyo vya biashara vinaondolewa.
“Tunajadiliana na nchi wanachama wenzetu namna ya kupunguza vipimo vya uzito wa magari barabarani, hususan ni kwa magari yanayosafirisha mizigo toka nchi moja kwenda nyingine,” alisema.