Na Dotto Mwaibale
KAMPUNI ya Vizimbuzi ya StarTimes Tanzania imetoa vizimbuzi 50 kwa bei ya sh.50,000 kwa vijiji vitatu vya Matimbwa, Chasimba na Yombo vilivyopo Bagamoyo mkoani Pwani. Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kukabidhi vizimbuzi hivyo kwa wananchi wa vijiji hivyo, Meneja Mauzo wa Kampuni hiyo Tang Jing Yu alisema lengo lao kubwa ni kusogeza huduma ya kidigitali kwa wananchi.
“Kampuni yetu imejipanga kuhakikisha inasaidia watu wa vijijini kupata huduma nzuri na kuwanufaisha katika mfumo wa kidigitali,” alisema Jing Yu.
Jing Yu alisema kwa awamu ya kwanza wameanza kwa kusambaza vizimbuzi 50 chini ya mradi huo katika vijiji hivyo ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Rais wao wa China za kusaidia nchi za Afrika kidigitali hasa katika maeneo ya vijijini.
Alisema China inajisikia fahari kubwa kuona wananchi wa Afrika wananufaika na mradi huo na kwa hapa Tanzania wameanza katika eneo hilo la Bagamoyo lakini lengo likiwa ni kuvifikia vijiji vingi zaidi. Ofisa Idara ya Masoko wa StarTimes, Furaha Mayala alisema kabla ya kuanza mradi huo waliwatembea wananchi na kuzungumza nao na kujionea changamoto kubwa ya kukosa mawasiliano hayo ya kidigitali.
Alisema kampuni hiyo imetoa vizimbuzi hivyo kwa watu 50 wa vijiji hivyo ambapo watatumia kwa kipindi cha mwezi mmoja bila ya kulipia na amewataka wananchi wengine kuchangamkia fursa hiyo. Mgeni rasmi katika hafla hiyo Ofisa Tarafa ya Yombo Rashid Kiwamba alisema kupelekewa vizimbuzi hivyo kwa bei nafuu ni fursa kwao hasa katika kipindi hiki cha sayansi na teknolojia ambapo dunia imekuwa ni kijiji kimoja.
Kiwamba alisema kwamba mradi huo uliopelekwa na StarTimes ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Dk.John Magufuli aliyoahidi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu za kuhahikisha huduma mbalimbali zinawafikia wananchi ikiwa ni pamoja na mawasiliano.
“Mradi huu tulioletewa na hawa ndugu zetu wa StarTimes ni mzuri na ni mwanzo mzuri na mambo mengi mazuri yanakuja hapa kwetu Yombo ni muhimu wananchi kuuchangamkia,” alisema Kawamba.
Mkazi wa Kijiji cha Chasimba Miraj Mukadase aliishukuru kampuni hiyo kwa kuwapelekea mradi huo ambao utawasaidia kupata taarifa mbalimbali kwa wakati.
“Tulikuwa tukikosa taarifa mbalimbali kwa kuwa tulishindwa kupata vizimbuzi vya bei nafuu na vilivyobora ambapo vilikuwa vikuzwa hadi sh.120, 000 lakini leo hii StarTimes wametukomboa tunawapongeza sana,” alisema Mukadase.