Na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Charles Kitwanga amesema Serikali itazima mitambo ya kituo chochote cha radio nchini ambacho kitakuwa kikirusha matangazo yake kwa mfumo wa analojia hadi ifikapo Disemba 31, 2012. Alisema baada ya hapo vituo vyote vya radio vitalazimika kurusha matangazo yake kwa kutumia teknolojia ya digitali.
Kitwanga ametoa kauli hiyo leo alipokuwa akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salam, huku akisisitiza kuwa mabadiliko hayo yanatokana na changamoto zinazozikabili teknolojia ya analojia ikiwemo uhafifu wa picha na sauti pamoja na matumizi makubwa ya masafa, nishati na teknolojia inayopitwa na wakati kiurushaji matangazo.
Aidha amesema kuwa maendeleo ya kiuchumi yanatokana na teknolojia bora zaidi ya mawasiliano hususani matumizi ya kifaa kimoja kupata huduma mbalimbali ikiwemo kuunganisha huduma za simu, intaneti na utangazaji ambayo hayawezi kufikiwa kwa mfumo wa teknolojia ya analojia.
Naibu huyo waziri ameongeza kuwa ili kukabiliana na changamoto hizo hasa katika kuwezesha watumiaji wa huduma hiyo nchi wanachama wa umoja wa kimataifa wa mawasiliano ikiwemo Tanzania zilikubaliana kwa pamoja kubadilisha mfumo wa utangazaji wa teknolojia ya analojia na kuanza kutumia teknolojia mpya ya digitali.