JESHI la Sudan Kusini limesema linajiandaa kufanya shambulio kubwa dhidi ya vikosi vya waasi wakati nchi hiyo inayoelekea kuingia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe licha ya juhudi za kimataifa za kutafuta suluhu.
Uwezekano wa kuzuka kwa mapigano makubwa umekuja wakati Umoja wa Mataifa ikionya kwamba hali katika taifa hilo jipya hilo changa kabisa duniani inatibuka kwa haraka ambapo hivi sasa mamia kwa maelfu ya raia wakiwa katika hatari. Inaripotiwa kwamba idadi ya vifo kutokana na machafuko ya umwagaji damu ya wiki iliopita inaweza kupindukia 1,000.
Mapigano yameikumba Sudan Kusini kwa zaidi ya wiki moja baada ya Rais Salva Kiir kumshutumu makamo wake Riek Machar kufanya jaribio la mapinduzi baada ya kumtimuwa kutoka serikalini hapo mwezi wa Julai.
Makamo wa Rais wa Sudan Kusini aliyetimuliwa Riek Machar amekanusha madai ya kuhusika na jaribio la mapinduzi na kumshutumu Kiir kwa kwa kuchukuwa hatua kali ya kuwaadhibu wapinzani wake. Machar ameapa kumuondowa Kiir madarakani na vikosi vyake tayari vimeuteka mji wa Bor ambao ni mji mkuu wa jimbo lenye vurugu la Jonglei ukiwa kama kilomita 200 tu kaskazini mwa mji mkuu wa Juba na pia wameuteka mji wa Bentiu ambao ni mji mkuu wa jimbo muhimu lenye kuzalisha mafuta la Unity.
Msemaji wa Jeshi la Sudan Kusini Philip Aguer amesema serikali imechukuwa hatua ya kufanya mashambulizi. Ameviambia vyombo vya habari kwamba wanajeshi wao wataukombowa mji mwa Bor kutoka kwa vikosi vya waasi na kwamba mji huo bado unadhibitiwa na vikosi vya Machar lakini wanajiandaa kuudhibiti tena mji huo.
Matamshi hayo yanakuja licha ya kuwepo kwa juhudi za kidiplomasia za mataifa ya Afrika na wito kutoka Marekani, Uingereza na Umoja wa Mataifa wa kutaka kusitishwa kwa mapigano hayo. Mratibu mkuu wa masuala ya misaada ya kibinaadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini Toby Lanzer ameutembelea mji huo wa Bor hapo jana na kusema kwamba hali inazidi kuwa mbaya. Amesema kuna maelfu ya raia wa Sudan Kusini waliokimbilia vichakani au kurudi kwenye vijiji vyao ili kuepuka madhara.
Ameongeza kusema ana wasi wasi mkubwa wa vita vinavyounyemelea mji huo ambapo amekiri kwamba ni jambo lisiloyumkinika kwa wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kuwa katika uwezo wa kuwalinda raia wanaokadiriwa kufikia 15,000 wanaotafuta hifadhi katika kambi ya Umoja wa Mataifa ilioko huko. Kwa mujibu wa Lanzer raia wa Australia, Uganda na Ethiopia ni miongoni mwa watu hao waliotafuta hifadhi katika kambi ya Umoja wa Mataifa huko Bor.
Ofisa huyo mwandamizi wa Umoja wa Mataifa pia amesema helikopta za kiraia zimewahamisha raia wa Marekani kutoka mji huo ulioshuhudia mashambulizi mazito ya bunduki za rashasha lakini kuna raia 3,000 wa nchi kama vile Canada, Uingereza na Kenya wanaoendelea kukwama katika mji huo.
Lanzer ambaye anatafuta msaada wa kifedha wa haraka kutoka Jumuiya ya Kimataifa amesema idadi ya wakimbizi wa ndani ya nchi inaweza kupindukia 100,000. Rais Barack Obama wa Marekani mwishoni mwa juma ametuma baruwa kwa viongozi wa bunge la nchi hiyo akiwajulisha kwamba huenda akachukuwa hatua zaidi za kijeshi Sudan Kusini ili kuwalinda raia wa Marekani, wafanyakazi na mali zao.
-DW