Na Joachim Mushi
MCHAKATO wa kujadili na kuandika Katiba Mpya unaendelea bungeni mjini Dodoma, licha ya kuwepo kwa mvutano na mgawanyiko wa makundi ya wabunge wa bunge maalumu wanaojadili Rasimu ya Pili iliyowasilishwa kwao. Wakati hayo yakiendelea viongozi, wanaharakati na wadau wa watoto wanapendekeza masuala ya haki za msingi za watoto yatambulike vizuri katika katiba ijayo.
Mwenyekiti wa Mtandao wa Mashirika yanayofanya kazi na Watoto Tanzania ambaye pia ni Mratibu Miradi, Kituo cha Watoto wa Mtaani cha Dogodogo Kigogo (Dogodogo Centre Street Children Trust), Sabas Masawe anashauri ibara ya 43 ambayo inataja haki za msingi za watoto iendelee kuwepo mpaka Katiba inakamilika na iboreshwe zaidi katika mchakato unaoendelea Bungeni. Nasema haya maana tayari kuna baadhi ya watu wameanza kuhoji kwamba kwanini hata watoto wanaingia kwenye katiba ilhali wao ni sehemu ya watu kama wazazi wao.
Anasema pamoja na kuingizwa kipengele cha mtoto kwenye rasimu ya pili ya katiba bado kuna mambo ambayo wao kama wadau wangependa yaingizwe tena hivi sasa katika mchakato wa majadiliano unaoendelea. Anasema baadhi ya mambo hayo ni kama umri wa mtoto mwenyewe kutaja wazi kwamba ni kuanzia umri gani.
“…Unaweza ukaangalia hili ni suala la msingi sana kutaja umri wa mtoto mwenyewe anayezungumziwa…kwa sisi wadau wa watoto tunashangaa sana kwa maana nyingine tunaona suala hilo ni kama linaongeza utata, kumuweka mtoto kwenye katiba ilhali umeshindwa kumtambua (kiumri) mtoto ni yupi ni sawa na vichekesho…tunashauri mtoto huyu umri utajwe wazi kuondoa utata…,” anasema.
Mfano ukisema wazee wana haki ya kutibiwa bure lazima useme huyu mzee anaanzia umri gani na kuishia wapi. Huwezi kusema wazee watibiwe bure alafu unashindwa kuainisha vitu vya muhimu kama umri wao, bila hivyo utaleta mkanganyiko wa tafsiri…ndiyo maana hata sasa mtoto anayetajwa tunataka tujue anaanzia umri gani na kuishia umri gani. Sasa hili pekee linatushangaza watu wasomi wanajadili bila kuliona hili.
Huyu mtoto akiingia kwenye mgongano katika sheria anashughulikiwa namna gani kwasababu hili linaweza kuwa na mgongano kama pia litashindwa kutajwa kwenye katiba chombo ambacho ni sheria mama ya nchi. Masawe anasema mambo mengine ambayo yanatakiwa kuainishwa ni pamoja na kuelekeza namna ya kuwawajibisha wazazi ambao wamekuwa wakikimbia majukumu yao ya kulea watoto na kuwapeleka katika vituo vya yatima eti kwa madai wamewashinda.
“Hapa tunataka ijulikane pia hawa wazazi ambao wamekuwa wakikwepa majukumu yao wanawajibishwa vipi…maana wengine tunawapelekea mtoto wake anatamka wazi kwamba mimi huyu mtoto amenishinda kabisa, sasa kama amekushinda nani wa kukulelea? Sasa watu kama hawa lazima ijulikane namna wanavyowajibishwa kwenye katiba au kama ni jukumu la Serikali katiba ieleze wazi ili iwe rahisi kumbana mtu kisheria,” anasema Masawe.Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Watoto na Jinsia wa Tanzania, Anna Maembe, anasema Serikali inawapenda watoto na ndiyo maana katika mchakato mzima wa kukusanya maoni ilizingatia kupata maoni ya kutosha kutoka kwa watoto wenyewe pamoja na wadau wengine wanaotetea haki za watoto.
Bi. Maembe anasema Ibara ya 43 katika Rasimu ya Pili imeweka wazi haki za watoto pamoja na kufafanua zaidi. “…Ibara ya 43(1) (a) na kuendelea hadi (g) inaongelea kabisa na kufafanua kwa kina haki ya mtoto…hii ni pamoja na kulindwa, kuelimishwa, kupatiwa huduma za afya na huduma zingine zozote muhimu ambazo zitamfanya mtoto akuwe na kufikia utimilifu ambapo naye awe mzalishaji na mwananchi mwema…,” anasema Bi. Maembe akizungumza na mwandishi wa makala haya.
Anasema katika mchakato wa kukusanya maoni wadau wamepewa nafasi ya kutosha katika kutoa maoni kwa ushirikiano na wabunge, wadau wengine wa watoto, pamoja na mabaraza ya watoto ambayo yapo kila wilaya kutoa sauti za watoto. Anasema anaamini ibara iliyopo sasa inayozungumzia haki za watoto itaboreshwa zaidi mara baada ya mchakato kufikia mwisho hivyo kutoka na mwongozo mzuri zaidi wa kutetea haki za kundi hilo la watoto.
“…Binafsi mi bado naamini kuwa mchakato wa katiba, mi naomba niseme hivi mchakato wa katiba ni nafasi nzuri sana ya kuweza kutetea haki za watoto wa Tanzania, kwa kuwa mtoto wa leo ndiyo mbunge wa kesho, kwa hiyo tusipoweka haki zake vizuri hata wabunge wetu wajao hawatakaa wakatimiza wajibu wao vizuri…kwa kuwa sisi wote tulianzia utotoni hadi kufikia hapa, kwa hiyo mchakato wa katiba ufanye mambo yote lakini haki za mtoto zionekane vizuri ili sheria zote za nchi ziweze kupata mwongozo kutoka kwenye katiba yetu inayokuja ambayo ni sheria mama kuweza kutoa haki kwa mtoto.
Hata hivyo anasema mbali na haki za mtoto kuzingatiwa katika Katiba inayokuja bado watoto wanapaswa kuzingatia kuwa haki inakwenda sawa na wajibu, hivyo nao wanapaswa kutimiza wajibu yaani wasome kwa bidii, wakubali kuelekezwa na sio wafanye mambo yao kinyume kwa kuwa wanajua haki zao zimezingatiwa.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Fatma Mwasa anaipongeza Serikali kwa kitendo cha kutoa msukumo wa kipekee kwa kuwaingiza watoto katika Katiba Mpya. Anaongeza kuwa Serikali ina kila sababu ya kufanya hivyo maana imeridhia mikataba ya kimataifa kulinda haki za msingi za watoto, ambapo katika mikataba hiyo imeainisha mambo ya msingi ya kuzingatia.
Haki ya kuishi, haki ya kupata elimu, haki ya afya haki ya kuudumiwa na kulindwa. Anasema kikubwa ambacho tukiweza kukifanya kikapitishwa katika katiba mpya ambacho kitasaidia kuongeza hatua ambayo Serikali imefikia ni kiongeza umri wa mtoto wa kike kuolewa. Akifafanua zaidi Mwasa anasema suala hilo limekuwa na ajenda kwa muda mrefu hasa tunapopigania masuala ya kijinsia, usawa na haki za watoto.
Anasema eneo hili la umri wa kuolewa limekuwa likizua mkanganyiko kwa wengi kwa kile upande mmoja sheria kuruhusu mtoto wa chini ya miaka 18 kuolewa, licha ya upande mwingine bado sheria nyingine inamtambua mtu chini ya umri wa miaka 18 ni mtoto.
“…Kimsingi eneo hili limekuwa likizua utata kwa baadhi ya makundi katika jamii…hasa baadhi ya viongozi wa dini wao wanasema mtoto wa Tanzania anamaliza elimu ya msingi akiwa na miaka 14 na hapo kama hakufanikiwa kuendelea na sekondari hubaki nyumbani bila kuwa na cha kufanya, wanasema mtoto huyu anaweza kujiingiza katika mchezo mbaya kama atakaa tu akisubiri umri wa kuolewa wao wanaona kama amepata wa kumuoa ni bora akaolewa kuliko kujikuta akijiingiza katika mambo yasiofaa,” anasema Mkuu wa Mkoa huyo.
Anasema hata hivyo anaishukuru Serikali kuleta shule za kata maana idadi kubwa ya watoto sasa wanapata nafasi za kuendelea na masomo na kujikuta wakiepukana na hatari za ndoa za utotoni, lakini pamoja na hayo anasema bado kuna haja ya kujenga mfumo mzuri wa kuhakikisha suala la ndoa za utotoni linatoweka kabisa. Pamoja na hayo anabainisha kuwa kuna haja ya Katiba kutamka wazi kuwa mtoto asiruhusiwe kuolewa chini ya umri wa miaka 18.
Akizungumzia haki kwa makundi maalum ya watoto wakiwemo walemavu, anawashauri wazazi wenye imani potofu kubadilika na kumchukulia mtoto mlemavu ana haki zote kama ilivyo kwa watoto wengine. Anasema baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwaficha watoto wenye ulemavu ili wasiweze kupata haki zao ya msingi.
“…Kwenye hili changamoto kubwa ilikuwa wazazi wenyewe kufikiri kuwa kuzaa mtoto mwenye ulemavu ni jambo ambalo linaleta fedheha, hii imekuwa ikisumbua sana maana wakati mwingine tunabaini watoto wenye ulemavu wakiwa wamewekwa ndani wakati mwingine kwa miaka kadhaa…sasa hili tunaamini sio haki maana mtu yeyote anaweza kuwa mlemavu wakati wowote hata mimi sasa kumbagua juu ya haki kwa kuwa yuko vile sio sawa hata kidogo,” anasema Mwasa.
Bi. Valerie Msoka ni Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA), anasema ili mabadiliko katika jamii yatokee vyombo vya habari vinahitajika sana na kwa namna yingine vinatoa mchango mkubwa. Anatolea mfano kuwa kwa sasa matukio ya ndoa za utotoni bado yanashamiri kwa baadhi ya mikoa kwa kiasi kikubwa. Anasema pamoja na vitendo hivyo kuendelea vyombo vya habari ndiyo nyenzo pekee ambayo inaweza kubadili mtazamo katika jamii na matendo hayo kukoma kabisa.
Anasema mijadala inayoendelea kutoka kwa jamii na vyombo vya habari kuendelea kuripo inasaidia wajumbe wa Bunge la Katiba kupata taarifa za kina zaidi juu ya masuala mbalimbali wanayoyajadili hivi sasa hivyo kuendelea kuboresha zaidi. “…Mfano masuala ya ndoa za utotoni yanayozungumzwa hivi sasa, ukeketaji na masuala mengine ya unyanyasaji wanayofanyiwa watoto na vyombo vya habari kuandika yanawasaidia wabunge kuwa naufahamu zaidi wanapochangia katika kamati mbalimbali za Bunge la Katiba…kwa maana hiyo mchango wa vyombo vya habari unaitajika sana,” anasema Bi. Msoka.
Anasema ili kuondoa utata juu ya umri wa mtoto; Katiba ijayo ingemsaidia mtoto kutamka wazi kuwa mtoto wa kike au wa kiume haruhusiwi kuoa au kuolewa akiwa chini ya miaka 18. Anasema hii ikitamkwa wazi watu wataelewa na hata utoaji elimu kwa jamii juu ya umri wa mtoto na haki zake hauta kuwa wa mkanganyiko kama ilivyo sasa.
Anasema kwa sasa zipo baadhi ya mila zinashindwa kumlinda mtoto hasa wa kike hivyo kujikuta wanaozeshwa na kukosa haki zao za msingi ya kupata elimu, ilhali sheria zinashindwa kuwasaidia kwa kile nayo kuwa wa utata juu ya umri wa kuolewa kwa mtoto. Anasema katiba mpya ikitamka wazi masuala hayo itakuwa rahisi kuwashughulikia wanaotumia udhaifu wa sheria na kumnyanyasa mtoto.
Hata hivyo anafafanua kuwa pamoja na kuweka sheria ya kumlinda mtoto katika hali zote za unyanyasaji bado jamii inatakiwa kupewa elimu ya kutosha juu ya kuziacha mila na desturi zilizopitwa na wakati ambazo zimekuwa zikimnyanyasa mtoto hasa wa kike. Mwanaharakati huyu ambaye pia ni Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba anashauri elimu ya kuanzia msingi hadi kidato cha nne itolewe bure na kwa watoto wote. Anasema mtoto atatakiwa kusoma hadi kidato cha nne bure kama ilivyo darasa la saba sasa kisha kuchujwa kidato cha nne.
“…Nasema hivyo nikiwa na sababu kwamba ukiangalia mtoto anayemaliza elimu ya msingi madarasa ambayo ni lazima kila mmoja apitie, wanamaliza wakiwa wadogo sana, sasa kwa hali hii mi ninashauri kuanzia msingi hadi kidato cha nne yangekuwa ni madarasa la lazima na bure ili watoto hawa wapate elimu hadi kidato cha nne angalau hapa watakuwa wameongeza kitu kichwani na miaka kusogea…,” alisema.
Anasema mtoto anayemaliza katika kidato cha nne angalau atakuwa amepata elimu kiasi, anajitambua na umri umeongezeka kidogo hivyo kama wengine wataishia katika darasa hilo wanaweza kujitegemea na hata walioolewa watajitambua hivyo kujenga familia ambazo zinajielewa kwa kiasi fulani tofauti na ilivyo kwa sasa.
Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Watoto na Jinsia wa Tanzania, Sophia Simba anasema takwimu zinaonesha kuwa Tanzania ni kati ya nchi 20 Ulimwenguni ambazo zimekithiri kwa kuwa na ndoa za utotoni. Aidha anabainisha kuwa takwimu pia zinaeleza katika kila watoto tano, wawili kati yao wameolewa chini ya miaka 18. “…Hili ni tatizo kubwa sana, fikiria kwa kila watoto watano wasichana wawili kati yao wameolewa chini ya miaka 18, sasa ukiangalia utaona karibuni kila wakati kuna mtoto anaolewa Tanzania akiwa chini ya miaka 18. Hili Serikali haiwezi kukaa kimya ndiyo maana kuna programu mbalimbali zinafanywa kukabiliana na hali hii…leo tumezinduwa kampeni za kukabiliana na hali hiyo Mara tutafanya hivi maeneo mengine pia kupinga suala hili,” anasema Bi. Simba.
Pili Muherisens (13) ni mwanafunzi wa darasa la tano katika moja ya shule za msingi Wilayani Tarime. Binti huyu alilazimika kutoroka kwao na kukimbilia eneo lingine akikwepa kukeketwa na wanaukoo kijijini kwao. Mtoto huyu wala wazazi wake wote hakupenda kukeketwa baada ya kuhofia madhara ya tendo hilo lakini ukoo ulishinikiza na ukatishia kama wazazi watazuia mtoto wao kufanyiwa hivyo wangeliwatenga na mama yake kupigwa. Hapo ndipo binti alipoamua kukimbia kijiji na kwenda kwenye vituo salama.
Binti huyu anaomba Serikali iwasaidie watoto kama hawa ambao hulazimishwa kukeketwa na hata kuozeshwa mapema ikiwa ni vitendo vya unyanyasaji dhidi yao. Cha kujiuliza ni watoto wangapi Tanzania ambao wanakumbana na unyanyasaji wa nguvu kama huu.