SIKU ya Jumapili (Machi 6, 2016) zaidi ya wanawake mia moja wanatarajia kujumuika pamoja jijini Dar es Salaam katika matembezi yaliyoandaliwa na Taasisi ya Vital Voices Global Partnership katika kuelekea siku ya wanawake duniani ambayo huadhimishwa Machi 8 kila mwaka duniani kote. Matembezi hayo yatashirikisha nchi 86 duniani ambayo yanalenga kuongeza viongozi wanawake kupitia semina na kupata mafunzo kutoka kwa wataalamu mbalimbali. Matembezi haya kwa mwaka huu yatabeba ujumbe wa usawa katika uongozi yaani 50% kwa 50% kwa wanawake na wanaume ifikapo 2030.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjumbe anayepeperusha bendera ya taasisi ya Vital Voices Global Partnership, Emelda Mwamanga alisema “mwaka huu matembezi haya yatahusisha viongozi katika nyanja mbalimbali kama vile viongozi wa serikali, wanawake wafanyabiashara, wagunduzi na waanzilishi wa taasisi mbalimbali za kijamii, wake wa wana siasa pamoja na wanaweke walioajiriwa katika taasisi mbalimbali. Tutaanza na matembezi ambapo wanawake watakaohudhria watapata wasaa wa kubadilishana mawili matatu huku wakitembea na baadae kutafuatiwa na semina itakayosaidia kuwaunganisha wanawake hawa waliotoka katika nyanja mbalimbali na kufanya majadiliano yatakayolenga kujikwamua kichumi.”
Aliongeza kwa kusema kuwa semina itakua na wazungumzaji mbalimbali mashuhuri kama vile Dr. Blandina Kilama atakayezungumzia maswala ya kiuchumi, Modesta Mahiga, Chris Mauki, Catherine Rose Baretto, Tausi na wengine wengi.
Mwamanga aliwashukuru sana wahisani waliowanga mkono kwa kudhamini matembezi hayo “shukurani za pekee kwa Jubilee Insurance kwa kuona umuhimu wa mwanamke katika jamii hata kukubali kudhamini matembezi haya. Kwa namna ya pekee pia napenda kwashukuru sana Total Ltd, M.J, Luv touch Manjano, Sheria Ngowi, Insight Consultant, Relim Media pamoja na Global peace foundation kwa udhamini mnono mliotupatia.”
Semina na matembezi hayo yatalenga kumjengea mwanamke mazingira ya kuongeza ulinzi na sapoti ambayo wanahitaji katika kukamilisha malengo yao. Kila Semina na dhumuni la Matembezi hayo hutofatiana kutokana na tamaduni na changamoto zinazowakabili wanawake wa nchi husika, lengo kubwa likiwa ni kugusa mahitaji ya wanawake katika jamii zao.
Matembezi haya kwa mwaka huu yatafanyika katika nchi zifatazo; Algeria, Argentina, Australia, Brazil, Cameroon, Costa Rica, Democratic Republic of the Congo, Ecuador, El Salvador, Ethiopia, Ghana, Guatemala, Haiti, Honduras, India, Israel, Jamaica, Jordan, Kenya, Lebanon, Liberia, Madagascar, Malaysia, Mali, Mexico, Myanmar, Namibia, Nepal, Nicaragua, Nigeria, Northern Ireland, Pakistan, Palestine, Panama, Papua New Guinea, Peru, Philippines, Poland, Saint Lucia, Serbia, Sierra Leone, South Africa, Spain, Tanzania, Thailand, Togo, Trinidad and Tobago, United Arab Emirates, Uganda, Ukraine, the United States, Uruguay, Vanuatu, Vietnam, Yemen, Zambia, na Zimbabwe.
Naye Meneja Masoko ktoka Jubilee Insurance Francisca Mshiwa aliwapongeza waandaji wa matembezi hayo na kuwahakikishia watakua pamoja katika mapambano ya usawa wa mwanamke katika uongozi na kuwataka wadau wengine wajitokeze kuwanga mkono viongozi wanawake wanaopigania haki na usawa kwa wanawake katika jamii nchini kwetu.