Na Mwandishi Wetu
TUME ya Maadili ya Utumishi wa Umma imesema urejeshwaji wa fomu za matamko ya madeni na mali za viongozi wa utumishi wa umma kwa kipindi hiki, mwitikio wa viongozi umeongezeka ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Katibu Mkuu wa Tume hiyo, Tixon Nzunda amewaeleza waandishi wa habari jana Dar es Salaam kuwa ongezeko la sasa ni la asilimia 22.5 tofauti na ilivyo kuwa awali.
Nzunda amesema kuwa idadi kubwa ya watumishi wa umma waliotumiwa fomu za madeni na mali walirejesha fomu hizo na kwamba kada ya viongozi wakuu wa serikali yaani Mawaziri, Manaibu Waziri, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Wakuu na Makatibu Tawala wa Mikoa walitii agizo hilo.
Hata hivyo, licha ya ongezeko hilo, Zunda ameeleza kuwa asilimia 26 ya viongozi wa utumishi wa umma hawakurejesha fomu hizo, akizitaja kuwa ni pamoja na kada za Mahakimu wa mahakama za mwanzo, Mabalozi na Madiwani.