MGOGORO wa uongozi ndani ya Chama cha Makatibu Muhtasi Tanzania (TAPSEA) umeingia katika hatua tata baada ya viongozi waanzilishi wa chama hicho kulalamikia uchaguzi uliopangwa kufanyika Mai 30, 2015 mjini Dodoma ilhali kuna mgogoro wa uongozi ndani ya chama hicho ukiendelea.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa niaba ya viongozi wenzake Mwenyekiti wa TAPSEA, Pili Mpenda ambaye pia ni miongoni mwa waanzilishi wa chama hicho jana jijini Dar es Salaam alisema anasikitishwa na kitendo cha viongozi walioingia kinyume na katiba ya chama hicho kujipanga kufanya uchaguzi ilhali kuna kesi ya msingi ipo mahakamani kulalamikia wao kuondolewa madarakani.
Alisema viongozi waliopo madarakani sasa wameingia kwa nguvu za Msajili wa Vyama vya Siasa nchini baada ya kushinikiza uchaguzi kinyume na maelekezo ya Mkutano Mkuu wa kwanza wa TAPSEA uliofanyika Arusha Mai 18, 2013 wa chama hicho ambao ulielekeza maboresho ya katiba ya chama kabla ya chochote kufanyika.
Alisema mkutano mkuu wa pili uliofanyika mkoani Mwanza 2014 uliitishwa ili kuwaeleza wananchama juu ya shinikizo la msajili na wanachama wachache (7) kufanyika uchaguzi na kuwaeleza mwenendo wa marekebisho ya katiba ya TAPSEA lakini Ofisa msajili alishinikiza ufanyike uchaguzi ambao uliwagawa wanachama na wengine kususia uchaguzi huo kutokana na mvutano.
Bi. Mpenda alisema uchaguzi uliofanyika haukuwa halali kwani mbali na kufanyika kinyume na katiba ya TAPSEA na maelekezo ya Mkutano Mkuu wa kwanza haukushirikisha wanachama wote. Aliongeza kuwa kati ya wanachama halali 815 waliokuwa wamejisajili ni wanachama 200 tu ndio walioshiriki katika uchaguzi huo.
“…Uchaguzi huu ni kinyume na katiba ya TAPSEA na kinyume na maelekezo ya Mkutano Mkuu wa kwanza na ulifanyika kwa shinikizo la Msajili wa Vyama vya Siasa…sisi hatujui alitumia kifungu gani kuja kushinikiza uchaguzi na kuusimamia kinyume na katiba yetu,” alisema Bi Mpenda katika mazungumzo.
Aidha alisema tayari viongozi waliopinduliwa wameenda mahakamani kupinga kitendo hicho na msajili anafahamu lakini wanashangaa kuona viongozi wanaolalamikia wamejipanga kufanya uchaguzi mpya wa chama hicho Mai 30, 2015 mjini Dodoma. Hata hivyo taarifa kutoka kwa viongozi waliopo madarakani kwa sasa wamekiri kujiandaa na uchaguzi mkuu mpya kwa nafasi za juu za chama hicho pamoja na wajumbe 9 wa Kamati ya Utendaji.
Akizungumza leo mjini Dodoma na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa TAPSEA aliyepo madarakani kwa sasa, Festo Emmanuel amesema chama hicho kinaendelea na mkutano mkuu unaoanza leo mjini hapo na wamesajili upya wanachama ambapo imefikia jumla ya wanachama 1500. Na alikiri watafanya uchaguzi katika nafasi za juu za chama hicho.
Viongozi wa TAPSEA walioko madarakani sasa ambao wanaolalamikiwa kuingia madarakani kinyume na katiba ya chama hicho wakizungumza na baadhi ya waandishi wa habari mjini Dodoma kuzungumzia mkutano wao mkuu unaoanza leo mjini Dodoma.