VIONGOZI wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) leo kwa pamoja wametia saini itifaki ya Umoja wa Fedha wa Afrika Mashariki, ( The East African Monetary Union) katika hoteli ya Speke, Munyonyo mjini Kampala. Marais waliotia saini itifaki kwa niaba ya wananchi wao ni Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania, Pierre Nkurunziza wa Burundi, Uhuru Kenyatta wa Kenya, Paul Kagame wa Rwanda na Yoweri Museveni wa Uganda .
Mara baada ya utiwaji wa saini, itifaki ya Umoja wa Fedha itapelekwa Kwenye mabunge ya nchi wanachama kwa ajili ya kuridhia ifikapo Mwezi Julai mwaka 2014. Utiaji wa saini huu unaanzisha mchakato wa kuelekea kuwa na sarafu moja ifikapo mwaka 2024 kwa nchi za Afrika Mashariki.
Kikao cha viongozi pia kilishuhudia Rais Kenyatta akichukua Uenyekiti wa Jumuiya kutoka kwa Rais Museveni na kuelezea matarajio yake ya Jumuiya kukua zaidi na kuzitaka nchi wanachama kuelimisha zaidi wananchi wa Afrika Mashariki kuhusu faida za Ushirikiano huu.
Itifaki ya Umoja wa Fedha ni ya tatu baada ya itifaki ya Umoja wa Ushuru wa Forodha na itifaki ya soko la pamoja na hatimaye kuelekea kwenye Shirikisho la Afrika Mashariki. Katika mkutano wa Leo, mbele ya viongozi wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, mwanafunzi Peter Robert kutoka shule ya sekondari Tushikamane, Morogoro amepokea cheti na zawadi ya fedha taslimu baada ya kuibuka mshindi wa shindano la kuandika Insha inayohusu EAC.
Mara baada ya kikao, Rais Kikwete amerejea jijini Mwanza kuendeleza na ziara ya kikazi katika Mkoa wa Simiyu ambapo kesho tarehe 1, ataendelea na ziara katika Wilaya ya Busega.