BAADHI ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Chadema kutoka Jimbo la Kawe wamekihama chama hicho na kukimbilia Chama cha ACT, Wazalendo. Akizungumza jana na wanahabari, Naibu Katibu Mkuu, ACT Wazalendo, Msafiri Mtemelwa alisema wamewapokea viongozi hao na kuwagawia kadi za chama chao.
Alisema tukio hilo la kupokea wanachama lukuki pia linaendelea katika mikoa mbalimbali nchini. Aliwataja viongozi toka Chadema Jumbo la Kawe waliojiunga na ACT ni pamoja na Diwani wa Kunduchi, Janeth Rithe, ambaye pia kabla ya kujiunga alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la wanawake (Bawacha) wa jimbo la Kawe, Mary Mongi ambaye alikuwa mjumbe kamati ya utendaji Bawacha Jimbo la Kawe na James Wambura aliyekuwa Katibu wa Mbunge Kawe (Halima Mdee).
Wengine ni pamoja na aliyekuwa mpambanaji katika kampeni za mbunge Halima Mdee, Manase Busa na Modesta Kalukula(Modesta Power) ambaye alikuwa ni Katibu wa Bawacha tawi la Wazo. Wengine ni Sizya Issa (Mwanachama), Yamoyo Salehe(Mwanachama), Sheilah Khamis(Mwanachama), Tabia Mohamed (Mwanachama), Fatuma Mikidadi, Ashura Salehe (Mwanachama) pamoja na Sophia Makoba.
“Ndugu waandishi wa Habari, kwa pamoja hawa wameungana nasi kwa ajili ya kuendeleza uzalendo kwa Taifa lao nasi tunawakaribisha. Tendo hili la leo la kuwakaribisha wanachama hawa ni muendelezo wa kuwatambulisha wanachama mbali mbali wakiwemo wabunge na viongozi wa vyama waliojiunga nasi baada ya kuvunjwa kwa Bunge.”
“…Tayari tunao baadhi ya watu waliokuwa wabunge na wameshajiunga nasi na mchakato wa kuwatambulisha unaendelea katika maeneo mbali mbali nchini na kesho wabunge hao wataanza kujulikana rasmi. Nawashukuru kwa kunisikiliza
Hata hivyo, Kiongozi wa Chama Zitto Kabwe, juzi mkoani alimpokea aliyekuwa mbunge wa Kasulu Mjini Moses Machali na wanachama wengine zaidi ya 1000. ACT Wazalendo imewataka wananchi na wakazi wa jijini Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la wapiga kura.
“…Sisi ACT-Wazalendo tunaamini bila ya kukiondoa chama hicho madarakani watanzania wataendelea kulalamika kila siku juu ya ufisadi, ubadhirifu na ukosefu wa huduma za msingi za kijamii ikiwamo haki ya msingi ya kupata huduma za afya zilizo bora kwa kila mmoja wetu. Hivyo basi tunawaomba wananchi watumie fursa hii adhimu kwao kuhakikisha wanajiandikisha na mwisho wanapiga kura kwa wagombea wanaowataka hasa wanaotokana na chama cha ACT-Wazalendo.” Alisema kiongozi huyo wa Cahadema.