Viongozi na Diwani CHADEMA Tarime waswekwa maabusu

Na mwandishi wetu
Tarime,

Viongozi wa ngazi ya juu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani Tarime pamoja na Diwani anayetokana na Chama hicho wamepelekwa maabusu hii leo baada ya kufikishwa katika Mahakama ya Wilaya kwa kudaiwa kutoa maneno ya uchochezi na kufanya fujo katika chumba cha kuhifadhia Maiti kaika hospitali ya Wilaya ya Tarime.

Mbele ya Hakimu mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Tarime Yusto Ruboronga inadaiwa June 5 mwaka huu washitakiwa hao wakiwa katika hospitali ya Wilaya ya Tarime waliwazuia ngugu wa marehemu kuuchukua mwili wa ndugu yao naoa maneno ya uchochezi wakidai kutaka kufanyiwa uchunguzi wa kina kabla kuzikwa ili kujua sababu ya kifo cha Mogosi Chacha.

Washitakiwa hao ambao ni Mwenyekiti wa Wilaya Lucas Ngoto,Katibu Mwita Mroni pamoja na Diwani anayetokana na Chama hicho cha (CHADEMA) wa kata ya Nyamisangura Christopher Chomete wanadaiwa kusababisha usumbufu katika hospitali hiyo ya Wilaya ya Tarime huku wakitoa maneno ya uchocheze juu ya tukio la kifo hicho cha Mogosi kilichotokea katika Mgodi wa Nyamongo.

Washitakiwa wote watatu wamekana mashitaka yao mara baada ya maelezo kutoka katika pande zote za mashitaka na kupelekwa maabusu hadi June 16 baada ya kunyimwa dhamana kutokana na kuhofia kurudi katika eneo la msiba kwenda kuendeleza kutoa maneno ya uchochezi dhidi ya ndugu wa marehemu.

Marehemu Mogosi Chacha aliuwawa kwa kupigwa risasi na askari wa jeshi la Polisi June 4 baada ya kudaiwa kuvamia katika Mgodi wa Nyamongo na kumjeruhi mlinzi wa mgodi huo Winchlaus Petro pamoja na kutaka kumkata askari na panga ndipo alipopigwa risasi ya pembeni ya mkono na kupitia ubavuni na kupelekea kifo chake.