Viongozi Chadema wafikishwa mahakamani kwa ujambazi

Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk Willbroad Slaa

Na Janeth Mushi, Arusha

KATIBU wa Baraza la Vijana wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) Wilaya ya Arusha, Anold Kamdye na aliyekuwa Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Arusha mjini, Gervas Mgonja, jana wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za ujambazi wa kutumia silaha.

Mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Agustine Kombe alidai kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa hilo Agosti 6 mwaka huu majira ya saa tatu usiku eneo la Ngarenaro Manispaa ya Arusha.

Mbele ya Hakimu, Rose Ngoka, Kombe aliieleza mahakama hiyo kuwa watuhumiwa hao ambao wakiwa na silaha (bunduki na bastola) ambazo walizitumia katika uhalifu huo.

Alidai kuwa watuhumiwa hao walivamia nyumbani kwa Elizabeth Makupa na kupora fedha taslimu sh. milioni 1.8, simu aina ya Samsung yenye thamani ya sh. 800,000 na Blackberry yenye thamani ya sh. 400,000.

Aidha upelelelezi juu ya kesi hiyo bado haiuajamilika na watuhumiwa hao bado wako chini ya ulinzi na kesi hiyo inatarajwia kutajwa Septemba 8 mwaka huu.