Viongozi Chadema waachiwa huru

Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo Taifa(Chadema), Benson Kigaila

Viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliokamatwa juzi kwa madai ya kuvunja amri ya polisi ya kutofanya mkutano wa hadhara, wameachiwa huru.

Viongozi hao wanane, wanachama wawili na dereva mmoja, waliachiwa juzi usiku baada ya kuwekewa dhamana na wanachama wenzao.

Walikamatwa kwa madai ya kuvunja amri ya kutofanya mkutano wa hadhara katika viwanja vya Barafu, mjini hapa.

Waliokamatwa na kuachiwa ni pamoja na Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo Taifa, Benson Kigaila, Katibu wa Mkoa, Steven Massawe, Katibu wa Wilaya, Jela Mambo, Mwenyekiti wa Wilaya, Edward Mgawe.

Wengine ni Mjumbe wa Baraza Kuu wa Taifa, Alex Nicholaus, mwanachama Khalid Zoya, Katibu wa Baraza la Wanawake Mkoa, Kunti Yusuph, Katibu wa Wanawake Wilaya, Magreth Thadei, Katibu wa Wazee Wilaya, Ahmed Sango, mwanachama Enock Mhembano na dereva, Juma Waziri.

Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo Taifa wa chama hicho, Benson Kigaila, alisema jana kuwa viongozi wote wa chama hicho waliokamatwa wameachiwa na polisi ingawa wamepewa masharti ya kutofanya mkutano wa hadhara.

“Walituambilia turudi tena leo (jana) saa 4:00 asubuhi na tulienda ili kuwasikiliza wanasemaje kama wanataka kutupeleka mahakamani watupeleke, au kama wanatuachia huru watuachie huru,” alisema.

Alisema walipofika kituoni hapo waliambiwa kuwa polisi watafanya upelelezi ili kugundua kama kuna ushahidi wowote wa kesi na wameahidi kuwa utakamilika Oktoba 25, mwaka huu.

Hata hivyo, Kigaila alisema polisi walivunja mkutano wao huo kwa maelekezo ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwa taarifa za kufanya mkutano huo zilipelewa tangu Oktoba 16, mwaka huu.

Aliongeza kuwa baada ya kupeleka barua hiyo walikaa siku mbili bila kufanya matangazo wakisubiri pingamizi lakini siku iliyofuata ambayo ni Oktoba 18, mwaka huu, walianza kutangaza kuwepo kwa mkutano huo kwenye viwanja vya Barafu.

“Sheria haikutupasa kusubiri lakini sisi kwa ustaarabu tuliamua kusubiri ili kama kuna lolote watuambie,” alisema.

CHANZO: NIPASHE