Vinara wa Makundi Kutoswa na CCM Mbio za Urais

Kinana akizungumza na wana-CCM leo mjini Sumbawanga, mkoani Rukwa

Na Bashir Nkoromo, Rukwa

KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, amesema CCM itamtosa bila haya mwanachama yeyote atakayeomba kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya CCM huku akiwa kinara wa kutegemea makundi kumwigiza katika nafasi hiyo.

Badala yake CCM itahakikisha mgombea inayemsimamisha ni mwana CCM asiyeendekeza makundi, mwadilifu ambaye kila akiteuliwa atakuwa hatiliwi shaka.

Kinana alisema hayo leo, wakati akijibu swali la mmoja wa wana-CCM katika mkutano wa wana CCM shina la Isesa mkoani hapa, akiwa katika ziara ya kujitambulisha yeye na sekretarieti mpya na kueleza usimamizi na utekelezaji wa ilani ya Chama.

Mwana CCM huyo,Peter Lilata aliitaka kujua CCM imejiandaa vipi kuhakikisha katika uchaguzi mkuu wa 2015, CCM inateua mgombea ambaye atakubalika na wananchi wengi, na kutofanye kosa kuteua mgombea ambaye hakubaliki kwa kuwa kufanya hivyo kutaisababishia usumbufu mkubwa CCM katika kupata ushindi.

Mapema akizungumza baada ya kuzindua shina hilo, ambapo alilichangia sh. 500,000 ili kujiimarisha, Kinana aliwataka viongozi wa CCM kuonyesha mfano wa ujenzi wa Chama kwa kutembelea ngazi za mashina na matawi.

“Kuanzia sasa tutawapima vionmgozi wetu kwa namna wanavyokuwa wepesi kutembelea mashina na matawi ya CCM , kwa sababu utaratibu huu ndiyo pekee utakaokiimarisha Chama, na si vinginevyo”, Kalisema Kinana na kuongeza;

“Kutokana na kutambua hilo na kwa kuwa ni maelekezo yaliyotokana na maazimio kwenye Mkutano wetu Mkuu uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma, ndiyo sababu baada ya kupatiwa wadhifa huu (Ukatibu Mkuu wa CCM) mimi na wenzangu tumeanza ziara hii, na kila ninapofika lazima nitembelee mashina na matawi ili kuwa mfano kwa viongozi wengine”.

Kinana alisema, litakuwa jambo la ajabu sana ikiwa yeye kwa nafasi yake ya Ukatibu Mkuu anatembelea mashina na matawi, viongozi wa ngazi zingine wasifanye hivyo.

Akizungumzia suala la rushwa,izengwe katika uchaguzi, Kinana aliwataka wana-CCM kuhakikisha katika kila chaguzi wanahangaika kuunga mkono wagombea ambao ni watendaji wazuri na wenye maadili safi badala ya kukumbatia wanaowapa rushwa.

“Lazima mjue kwamba, mnapoamua kumchagua mgombea anayewapa rushwa, mnafanya kosa kubwa sana kwenu, maana akishapita anakuwa kiongozi wa kutetea maslahi yake na siyo yenu”, alisema Kinana.

Alisema, pamoja na kuwepo viongozi wanaotoa rushwa kutafuta uongozi, lakini, wananchi nao wamekuwa chanzo cha kukomaza rushwa kwa sababu mwanachama mwenzao anapojitokeza kuomba uongozi, huwa wa kwanza ‘kutengeneza’mazingira ya kumtaka atoe rushwa huku wakionyesha kwamba hawezi kupenya asipofanya hivyo.

Kinana alaiwataka wana-CCm kuacha kutungiana fitina, mizengwe na kuachana na makundi kabisa kila baada ya chaguzi kwa sababu mambo hayo yanachangia kwa kiasi kikubwa kudhoofisha mshikamano na umoja ndani ya chama ambao ndiyo siri ya ushindi.

Kinana ambaye katika ziara hiyo anafuatana na Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Nape Nnuauye na Katibu wa NEC, Oganaizesheni Mohamed Seif Khatib na baadhi ya mawaziri, aliwasili Rukwa leo akitokea mkoani Mtwara ambako alifanya mikutano kadhaa na kutembelea mashina na matawi ya CCM.