WAZEE wawili wakazi wa mji wa Namanyere wilayani Nkasi mkoani Rukwa,
wameandika historia ya pekee kwa kufunga ndoa wakiwa na umri mkubwa isivyo kawaida.
Wazee hao Mathias Kisokota (94) na Uria Mwimanzi (80) ambao wamefunga
ndoa hiyo ya kihistoria katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Antony,
parokia ya Namanyere wilayani Nkasi mkoani Rukwa.
Ibada ya ndoa hiyo iliyofungwa jana, iliongozwa na Mapadri wawili
ambao ni Paroko wa parokia hiyo, Padri Katindi na Twamba Peter ambapo
iliyovuta hisia za watu wengi kiasi cha kufurika katika kanisa hilo
kwa lengo kushuhudia wazee hao wakifunga ndoa.
Kabla ya Ibada hiyo kufanyika nyakati za saa 9 mchana gumzo katika mji
wa Namanyere, Sumbawanga na Mpanda ilikuwa ni juu ya kufungwa kwa ndoa
hiyo ambapo wakazi wa mjini humo wasikika wakieleza kuwa hii itakuwa
historia kwa wazee kufunga ndoa wakiwa na umri mkubwa kiasi hicho.
Wazee hao ambao wamefunga pingu za maisha kwa kuamua kuwa mwili mmoja
kama maandiko ya vitabu vya dini yanavyoeleza, wana watoto wapatao
kumi, na wajukuu zaidi 50 ambapo walianza kuishi pamoja miaka 35
iliyopita baada ya kufariki mke wa kwanza aitwaye Agnes Kasinsila.
Hata hivyo baada ya mzee Kasokota ambaye ni Mkatoliki kuanza maisha
mapya Uria anayesali Kanisa la Moravian mpaka sasa kufiwa na mkewe wa
kwanza, waliendelea kusali kama kawaida lakini wakikosa baadhi ya
huduma za kanisa.
Katika Mahubiri yake kanisani hapo, Padri Peter Twamba alisema kuwa
hiyo ni changamoto ya uokovu hasa kwa vijana kubadilika kitabia na
kutenda matendo mema na ya kumpendeza mwenyezi mungu hasa kipindi hiki
ambacho jimbo katoliki Sumbawanga linajiandaa kusherekea jubilei ya
miaka 125 tangu kuanzishwa kwake.
“Hii ni changamoto ya uokovu hasa kwa vijana kubadilika kitabia na
kutenda matendo mema ya kumpendeza mungu….. ni faraja kwetu katika
umri wa wazee hawa wameamua kufanga ndoa, tena kipindi ambacho
tunajiandaa kusherekea jubilei ya miaka 125 tangu kuanzishwa kwa jimbo
letu” alisema Padri Twamba.
Kwa mujibu wa Mjomba wazee hao ambaye ndio msemaji wa familia hiyo,
Filibert Lumbert, wazee hao pamoja na kwamba wameanza kupoteza baadhi
ya kumbukumbu muhimu katika akili zao lakini walisisitiza kila mara
kwamba lazima wafunge ndoa kanisani ili waweze kupata huduma zote
muhimu za kanisa kama ilivyo kwa wakristo wengine hususani wakatoliki.
Huduma ambazo wamekuwa wakizikosa ni pamoja kupokea mwili wa Kristu
(Sakramenti takatifu) na pia waliamini wakiendelea na maisha ya bila
ndoa wanaweza kuzikwa nje ya makaburi ya wakristo wakatoliki kitu
ambacho si sahihi kwao.
Hata hivyo ndoa ya wazee hao ambayo ilifana sana, sherehe zake
hazikuishia kanisani lakini badala yake zilikwenda hadi ukumbini
ambako watu waliwapongeza kwa kuamua kufanya tendo hilo muhimu katika
maisha ya wanadamu.
CHANZO; Gazeti la Jambo Leo