Na Fredy Mgunda, Iringa
VIJIJI 31 vilivyopo Mufundi Kaskazini mkoani Iringa vinatarajia kupokea umeme na tayari baadhi ya vijiji hivyo vipo katika hatua ya mwisho ya kufunga vikombe kwa ajili ya kuanza kuvuta nyaya za umeme.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Babtist Mdende amesema kuwa, vijiji vinavyotarajia kupata umeme safari hii ni vile vilivyopo Tarafa ya Sadani, Ifwagi na Kibengu.
“Vijiji hivyo ni Mapogoro, Igomaa, Kibada, Ndolezi na vingine vikiwemo Ugesa, Vikula, Ilasa na Kipanga ambavyo upimaji bado unaendelea kwa ajili ya kusimika nguzo. “Kuna baadhi ya vijiji vipo katika hatua ya awali ya kusimamisha nguzo ikiwepo Kijiji cha Isalavanu ambacho mradi wake wa umeme unashughulikiwa na TANESCO Wilaya ya Mufindi,” alisema Mdende.
Aidha Mdende ameeleza kuwa kwa wale watakao ingizwa kwa mara ya kwanza yaani watu wa kwanza wakati wa kuzindua mradi wa umeme wataingiziwa kwa gharama ya shilingi elfu 30.