Vijiji 150 vyakumbwa na njaa Nzega

Na Mwandishi Wetu
Nzega

WAKAZI wa wilaya ya Nzega pamoja na vitongoji vyake vimekumbwa na gharika kubwa la njaa, baada ya mvua za masika kutonyesha kikawaida.

Kutokana na hali hiyo sehemu mbalimbali za wilayani hapa zimekumbwa na ukame uliyosababisha njaa kwa wakazi wa vijiji anuai.

Wilaya ya Nzega ndiyo iliyoathirika zaidi kwani takribani vijiji 150 vimekumbwa na njaa na sasa vinaitaji msaada wa haraka.

Taarifa hizo zilitolewa jana na Mbunge wa Jimbo la Bukene, Selemani Zeddy katika kikao cha Baraza la Madiwani wilayani Nzega.

Alisema Baadhi ya wananchi wilayani hapo kwa sasa wanaishi kwa kupata mlo mmoja, jambo ambalo linatishia amani kulingana na hali halisi ya wahanga.

Alisema janga hilo linaikabiri wilaya yote ya Nzega hivyo na kuongeza kuwa jitihada za makusudi zinahitajika ili kunusuru wananchi na adha hiyo.

Hata hivyo akifafanua zaidi, Zeddy alisema Zaidi ya tani 262 zimetengwa kwa wilaya ya Nzega katika Ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha maafa zitakazo weza kusaidia kwa wakazi hao ambao mpaka sasa wanakabiriwa na janga hilo.

Serikali mkoani hapo ilitoa tahadhali mapema kwa kuwashawishi wananchi kulima zao la mtama na endapo wangelima kulingana na maelekezo hali isingelikuwa mbaya kama ilivyo sasa.